Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 22 Julai, 2025 ametembelea mradi wa maji wa Tarime/Rorya na kukutana na Mkandarasi, Mkandarasi Mshauri pamoja na msimamizi mkuu wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kufanyakazi usiku na mchana kukamilisha mradi huo.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo ambayo ilionyesha kuwa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 14.5 mpaka sasa na kumtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa.
“Sisi viongozi tutakuwa tunatembelea mradi huu usiku na mchana na eneo lolote unapotekelezwa ili kujiridhisha kuwa kazi zaukamilishaji wa mradi huu zinaendelea wakati wote, na tutachukua hatua kama kuna uzembe wa aina yoyote” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtambi amewataka wote wanaohusika na usimamizi wa mradi huo kuhakikisha kuwa kasi ya utekelezaji wa mradi huo inaridhisha na kama kuna changamoto kutoa taarifa kwa viongozi mara moja.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) Mhandisi Nicas Mugisha amesema mradi huo ulianza tarehe 23 Januari, 2023 na unatarajiwa kukamilika Septemba, 2026 kwa gharama ya shilingi bilioni 134.
Mhandisi Mugisha ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mradi huo amesema mpaka sasa mkandarasi wa mradi huo amelipwa malipo ya awali na malipo mengine ya awamu mbili na jumla ya shilingi 24,413,789,082 na mkandarasi haidai Serikali lakini utekelezaji wa mradi huo unaenda taratibu sana.
“Mradi huu ni muhimu kwa kuwa ukikamilika utaimarisha upatikanaji wa maji kwa wakazi 729,496 wa vijiji 37 za Wilaya ya Rorya na Tarime” amesema Bwana Mugisha na kuongeza kuwa mpaka sasa mradi umeajiri Watanzania 115 na waajiriwa wanatarajiwa kuongezeka hadi kufikia 819 kwa kadiri mradi unavyoendelea kutekelezwa.
Mhandisi Mugisha amesema shughuli kubwa iliyofanyika ni ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lita milioni tatu eneo la Mogabiri ambalo limekamilika, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lita milioni moja eneo la Sirari na Kituo cha kusukuma maji Gamasara pamoja na chujio la maji katika chanzo cha mradi huo unaendelea.
Kwa upande wao Meneja wa Mradi Adam Zhu kutoka kwa Mkandarasi wa mradi huo China Civil Engineering and Construction Corporation (CCECC) amekiri ucheleweshaji katika utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa hadi kufikia Desemba, 2025 kampuni hiyo itakuwa imekamilisha ujenzi wa miundombinu yote mikubwa katika chanzo cha maji Nyamagaro, Rorya na
Bwana Adam Zhu amesema kuwa kuwa mradi huo umechelewa kwa sababu mkandarasi alichelewa kupokea fedha na kuchelewa kwa baadhi ya vifaa vilivyoagizwa ambavyo kwa sasa vimeshafika Bandari ya Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara ametoa hadi tarehe 30 Agosti, 2025 Halmashauri ya Mji wa Tarime kufanya maboresho madogo madogo katika Shule ya Sekondari ya Tarime na kufuatilia maombi ya mabweni ya nyongeza katika shule hiyo ili kutatua changamoto za wanafunzi.
Mhe. Mtambi ametoa maagizo hayo baada ya kukagua na kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wa kidato cha sita katika shule hiyo ambao walimweleza kuhusiana na changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa mabweni, matundu ya vyoo, taa madarasani, meza na viti na upungufu wa maji.
Mhe. Mtambi ameitaka shule hiyo kuanzisha mfumo ambao utawawajibisha wanafunzi watakaobainika kuhusika na upotevu wa taa madarasani kwa kuanzisha mfumo wa kutambua wanaotumia vyumba vya madarasa kila wakati ili vifaa vinapoibiwa wawajibishwe.
Akiwa shuleni hapo Mhe. Mtambi amewataka wanafunzi hao kubadilika na kulinda vifaa vya shule kwa manufaa yao na amemuagiza Mkurugenzi wa Mjia wa Tarime kutoa pilau na nyama kwa wanafunzi hao siku ya Jumamosi na Jumapili za wiki hii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime Mwalimu Maro Chenge amesema mapungufu hayo kwa kiasi kikubwa yametokana na ongezeko la wanafunzi kutoka uwezo wa awali 780 hadi 932 waliopo sasa katika shule hiyo.
Mwalimu Chenge amesema kwa sasa shule inaupungufu wa viti na madawati 195 na ili kukabiliana na upungufu huo na ili kama jitihada za dharura za kukabiliana na upungufu huo, wanafunzi wamepewa mabenchi ambayo wanakalia kwa sasa.
Aidha, kuhusu taa, Mwalimu Maro amesema shule imekuwa inafunga taa ambazo zinaibiwa mara kwa mara jambo ambalo linasababisha madarasa mengi kukosa mwanga wa kutosha kutokana na kuwa na taa chache.
Mhe. Mtambi ametembelea maeneo hayo ikiwa ni sehemu ya ziara ya Kamati ya Usalama ya Mkoa kutembelea Wilaya za Rorya na Tarime kukagua miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 15-23 Agosti, 2025.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya, Kamati ya Wataalamu ya Mkoa, Wakuu wa Taasisi za umma, Menejimenti na watumishi wa Halmashauri za Rorya, Mji wa Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa