Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki kikao cha Baraza la Madiwani maalum kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na kuitaka Halmashauri hiyo kuongeza jitihada katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtambi amesema mwenendo wa makusanyo ya mapato ya ndani katika Halmashauri hiyo hauridhishi na kuongeza kuwa hadi kufikia tarehe 30 Mei, 2025 Halmashauri hiyo ilikuwa imekusanya asilimia 73 tu ya mapato yaliyotarajiwa kukusanywa katika mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ninatoa hadi tarehe 9 Juni, 2025 Halmashauri iwasilishe mkakati utakaoiwezesha kukusanya kwa asilimia 100 mapato ya ndani ifikapo tarehe 30 Juni, 2025” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema Halmashauri hiyo imekusanya shilingi bilioni 2.6 tu kati ya shilingi bilioni 3.6 ya lengo la mapato ya ndani na kuitaka Halmashauri hiyo kujipanga vizuri ili kuboresha makusanyo ya Halmashauri.
Kanali Mtambi pia ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi ya ukaguzi kwa miaka mitano mfululizo na kulitaka Baraza la Madiwani kwa kushirikiana na Menejimenti ya Halmashauri hiyo kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kusaidia Halmashauri kuweza kujiendesha na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowele amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo.
Meja Gowele amelipongeza Baraza hilo kwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano na kufanikisha azma yao ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Mji wa Tarime na kuongeza kuwa anawaombea kwa Mwenyezi Mungu waweze kuteuliwa tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Aidha, amewashukuru kwa ushirikiano wa Baraza la Madiwani kwa ofisi yake, Menejimenti na taasisi nyingine za Serikali katika Wilaya hiyo na kuahidi kuwa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wameyachukua kwa utekelezaji na hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2025 mapato yatakuwa kwenye wastani mzuri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Mhe. Daniel Komote amesema wakati wanaingia Halmashauri ilikuwa na bajeti ndogo sana na fedha zilikuwa zinakusanywa kwa kiasi kidogo chini ya asilimia 80.
Mhe. Komote amesema kwa sasa Halmashauri imeongeza makusanyo na kwa mwaka huu 2024/2025 walipanga kukusanya shilingi bilioni 3.6 na hadi kufikia tarehe 30 Mei, 2025 walikuwa wamekusanya shilingi bilioni 2.6 ambayo ni sawa na asilimia 73 ya bajeti yao.
“Hii fedha tunategemea kuikusanya ndani ya wiki mbili baada ya wafanyabiashara kulipia gharama za kukodi vibanda katika soko jipya la Tarime lililokamilika na makusanyo yake yalipangwa katika bajeti iliyopo” amesema Mhe. Komote.
Mhe. Komote amesema awali Halmashauri ilikuwa haina mradi mkubwa wa kuimarisha mapato ya ndani ya Halmashauri na baada ya soko la kimkakati kukamilika Halmashauri inategemea kuongeza zaidi ya milioni 500,000 kwa mwaka kutokana na mrdi huu.
Mhe. Komote amesema Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Tarime katika kipindi chake cha miaka mitano limeacha alama kubwa kwa kujenga miradi mipya ya kutolewa huduma ya afya, elimu na kadhalika kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kwa upande wake, Mwekahazina wa Halmashauri ya Mji wa Tarime CPA George Adino amesema katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ilikuwa na jumla hoja 70 na baada ya kuwasilisha majibu hoja 36 zimefungwa na 34 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
CPA Adino mesema kati ya hoja hizo hoja 27 ni mpya na katika hizo hoja 12 zimefungwa na hoja 15 zinaendelea kujibiwa aidha Halmashauri ilikuwa na maagizo matatu kutoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo yapo katika hatua za utekelezaji.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Tarime, baadhi ya maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Madiwani na Menejimenti ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa