Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha makusanyo yanapelekwa benki mapema ili kupunguza hoja za ukaguzi.
Mhe. Mtambi ameeleza hayo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza Maalum la Madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na kumtaka Mkuu wa Wilaya na Baraza kusimamia upelekwaji wa makusanyo benki. .
“Mkurugenzi hakikisha hamna fedha mbichi (fedha iliyokusanywa kabla ya kufikishwa benki) inayotumika, fedha zote ziende benki mara baada ya makusanyo, zisikae kwenye mikono ya watu” amesema Mhe. Mtambi .
Kanali Mtambi amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kusitisha mabadiliko ya Mhasibu wa Mapato katika Halmashauri hiyo hadi fedha zote ambazo zilikusanywa na kutokuwasilishwa benki ziwe zimerejeshwa.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuwasilisha kwenye Baraza la Madiwani orodha ya biashara zote zilizofungwa ili wafanye uhakiki wa uhalisia wa madai ya biashara zaidi ya 2,000 kufungwa katika Halmashauri hiyo jambo ambalo lilipingwa na baadhi ya madiwani walioongea.
Aidha, Mhe. Mtambi ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kufuatilia kesi za wakusanya mapato ambao hawajawasilisha fedha benki na kusababisha hoja ya ukaguzi.
Mhe. Mtambi ameitaka halmashauri hiyo kupanua wigo wa vyanzo vya mapato kulingana na mazingira ya Halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuwavutia watalii na wafanyabiashara kuwekeza katika Halmashauri hiyo.
Awali, CAG alihoji makusanyo kutokuwekwa benki kiasi shilingi 102,860,351 hata hivyo menejimenti ilieleza kuwa shilingi 22,382,030 zilikuwa zimerejeshwa na kuwekwa benki; shilingi 44,180,836 zimeombewa kufanyiwa marekebisho yaliyokuwa yametokana na dosari za mfumo wa mapato (LGRCIS) na kiasi 36,297,485 hakijawekwa benki.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa wahusika wa shilingi 11,128,450 kesi yao ipo katika uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU) na wahusika wa shilingi 25,169,035 wamepewa muda hadi kufikia Juni 30, 2024 wawe wameweka fedha zote benki.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa