Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 24 Juni, 2024 amelitaka Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kusimamia urejeshwaji wa shilingi bilioni moja zilizokopwa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutekeleza mradi wa Kupanga, Kupima na Kumirikisha ardhi (KKK) katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo wakati aliposhiriki Baraza Maalum la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) za mwaka 2022/2023 lililofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
“Halmashauri iweke mpango makakati wa kurejesha deni hilo ili kujenga mahusiano mazuri na kupata uwezekano wa kukopa tena huko mbeleni ” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi pia amekumbushia agizo lake la kumrejesha Afisa Ardhi aliyehamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kurejea Rorya kujibu hoja za ukaguzi zilizotokana na utekelezaji wa mradi wa KKK katika Halmashauri hiyo.
Kanali Mtambi amewataka madiwani kuvuta subira wakati Katibu Tawala wa Mkoa akiendelea kumfuatilia mtumishi huyo ambaye aliahidi kurepoti katika Halmashauri hiyo tarehe 24 Juni, 2024 kuja kujibu hoja za ukaguzi.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha manunuzi yanafanyika kupitia mfumo wa NEST na Baraza la Madiwani na watendaji wanapata mafunzo ya mfumo na Sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni zake ili manunuzi ya umma yafanyike kwa kufuata sheria.
Mhe. Mtambi amelitaka Baraza la Madiwani kusimamia lipaji mikopo ya madiwani katika benki za NMB na CRDB ambazo zilikatwa katika malipo ya kawaida ya madiwani lakini hayakupelekwa katika benki hizo kulipa mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Gerald Kusaya ameeleza kuwa mhusika alipewa maagizo ya kurejea Rorya kwa ajili ya kujibu hoja hata hivyo hakurejea na badala yake alileta barua yenye maelezo kuwa alikuwa anaumwa na kutoa maelezo mbalimbali kuhusu hoja za ukaguzi kuhusu mradi huo.
Bwana Kusaya ameeleza kuwa mara ya mwisho alipoongea nae aliahidi kurepoti Halmashauri ya Wilaya ya Rorya tarehe 24 Juni, 2024 kwa ajili ya kusaidia kujibu hoja za ukaguzi kuhusu mradi huo na kuahidi kuwa asipowasili siku hiyo Mkoa ungemchukulia hatua za kiutumishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mheshimiwa Gerald Ng’onga ameomba Afisa Ardhi huyo arejeshwe Rorya ili aisaidie Halmashauri hiyo kujibu hoja za mradi wa kupanga, kupima na kumirikisha ardhi (KKK) uliotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ng’ong’a amesema kutokana na mradi huo Halmashauri ilipata hoja za ukaguzi 21 kutokana na mradi wa KKK na kati ya hoja hizo 14 zimejibiwa na kufungwa lakini bado hoja saba hazijafungwa.
Kwa upande wao madiwani wa Halmashauri hiyo waliopata nafasi ya kuzungumza walielezea kusikitishwa kwao na kitendo cha Afisa Ardhi huyo kuchelewa kuwasili na kuendelea kukamishwa majibu ya hoja za mradi huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa