Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 25 Julai, 2025 amewapokea na kufanya mazungumzo na viongozi wa Shule za Feza za Jijini Dar es Salaam na kuwahamasisha viongozi hao kujenga Shule ya Feza katika Wilaya ya Butiama.
Akizungumza na viongozi hao, Mhe. Mtambi amesema Butiama ni eneo sahihi la kuwekeza katika masuala ya elimu kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mchango wake katika maendeleo ya elimu ya Tanzania.
“Ninawashauri mjenge Shule hii katika Wilaya ya Butiama, eneo ambalo mazingira yake ni mazuri kwa kujenga taasisi za elimu na ili kumuuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na mchango wake katika elimu ya Tanzania” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amezitaja sababu nyingine za kupendekeza Wilaya ya Butiama ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kujenga Chuo Kikuu cha Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia, Butiama (MJNUAT) ambapo Serikali imewekeza zaidi ya bilioni 102.5 na ujenzi wake upo katika hatua za ukamilishaji.
Aidha, Mhe. Mtambi amesema Mkoa pia umepeleka Shule ya Sekondari ya Amali ya Mkoa wa Mara inayojengwa katika Wilaya na kuongeza kuwa eneo hilo linafikika wakati wote kutokana na uwekezaji wa Uwanja wa Ndege Musoma na Barabara za lami zilizojengwa katika eneo hilo.
Mhe. Mtambi amesema kutokana na uwepo wa Chuo Kikuu cha MJNUAT itakuwa rahisi kwa Shule hiyo kupata wanafunzi watakaosoma katika shule hiyo kutokana na uwepo wa migodi, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwa jirani na mpaka wa Tanzania na Kenya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule za Fedha Bwana Ally Nungu amesema viongozi hao wametembelea mikoa ya Kanda ya Ziwa kuangalia uwezekano wa kujenga Shule ya Feza katika mkoa mmoja kati ya hiyo.
“Mapendekezo haya yatawasilishwa kwa viongozi na wamiliki wa Shule za Feza na viongozi wa juu wataamua Shule hiyo itajengwa katika Mkoa gani kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa tuliyoitembelea” amesema Bwana Nungu.
Aidha, Bwana Nungu amesema wataitembelea Wilaya ya Butiama na kuona uwezekano wa kuanza mazungumzo kwa ajili ya kupata eneo la ujenzi wa shule hiyo kama wamiliki wa shule hizo wataridhia Shule ijengwe Butiama.
Viongozi wengine waliokuwepo katika msafara huo ni Makamu Mwenyekiti wa taasisi ya ISHIK Foundation ambayo inamiliki shule za Feza na Mkurugenzi wa Mahusiano wa Shule za Feza Bwana Almas Mukanov.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa