Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi leo amefanya kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na kuwawataka Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu Wakuu wa Shule za msingi kuboresha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba na kidato cha nne.
“Kidato cha Sita mnafanya vizuri lakini shule ya msingi na kidato cha nne bado kunajitihada zinahitajika kuboresha elimu ya watoto wetu” amesema Mhe. Mtambi na kuwataka Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuchukua hatua kurekebisha hali hiyo.
Mhe. Mtambi amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Butiama kuwafuatilia Afisa Elimu Sekondari na Afisa Elimu wa Shule za Msingi ili wazisimamie shule zilizopo katika Halmashauri hiyo ili ziweze kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Mhe. Mtambi amemtaka Mkuu wa Wilaya kuitisha kikao cha wazazi wote katika shule za umma ambazo hazina mwitikio wa kuchangia chakula shuleni na fedha za taaluma kwa ajili ya kuwalipa walimu wa kujitolea na kuwahamasisha kuchangia michango hiyo ili shule hizo ziweze kufanya vizuri.
Kanali Mtambi amesema ofisi yake itaanza kutoa tuzo ya vinyago kwa shule ambazo zinafanya vizuri na ambazo hazifanyi vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa ili kutoa motisha kwa shule hizo kufanya vizuri katika mitihani inayofuata.
Wakati huo huo, Mhe. Mtambi amewataka walimu kukemea vitendo vichafu vinavyofanywa kwa wanafunzi mashuleni na kuwataka walimu kuwalinda, kuwaelimisha na kufuatilia tabia za wanafunzi wao na kama kuna mabadiliko toeni taarifa mapema.
Mhe. Mtambi amesema kuna taarifa za uwepo wa vitendo vya ushoga, ubakaji na ulawiti katika baadhi ya shule na katika jamii zikiwahusisha watoto wanaosoma jambo ambalo amesema halikubaliki, na kuwataka walimu wafuatilie wanafunzi wao.
Kwa upande wake, Mwalimu mkuu wa Sekondari wa Shule ya Sekondari ya Butiama Bibi Grace Isomba amesema kuwa mwaka 2021 shule yake ilipata ufaulu wa asilimia 87, mwaka 2022 asilimia 87 na mwaka 2023 walipata asilimia 84 .
Bibi Isomba ameeleza kwa mwaka 2023 ufaulu ulishuka kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi katika shule hiyo na kupungua kwa idadi ya walimu na baadhi ya wanafunzi kutoka maeneo ya mbali na shule hiyo mambo ambayo yaliathiri taaluma katika shule hiyo.
Bibi Isomba amesema kuwa changamoto nyingine katika shule hiyo ni asilimia kubwa ya wanafunzi kutopata chakula cha mchana shuleni kwa sababu wazazi wao hawajachangia chakula jambo ambalo linaathiri ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi hao.
Bibi Isomba amesema kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,242 hata hivyo wanafunzi wanaopata chakula cha mchana shuleni ni takriban wanafunzi 400 tu kwa shule nzima na wanafunzi waliobakia hawapati chakula na hivyo kushinda na njaa.
Akiwa katika Wilaya hiyo, Mkuu wa Mkoa alikagua mradi wa maji Kirumi, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, barabara za Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Kata ya Butiama, alifanya kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na kuhitimisha na mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Butiama.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ameambata na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Kamati ya Usalama Wilaya ya Butiama, Mwenyekiti na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Butiama baadhi ya maofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na watumishi wa Halmashauri ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa