Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi leo amempokea na kuzungumza na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bwana Yusuph Juma Mwenda na kuishauri mamlaka hiyo kuwasaidia wafanyabiashara kukuza na kuimarisha biashara zao.
Akizungumza na watendaji wa TRA na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara walioshiriki mapokezi hayo, Mhe. Mtambi amesema biashara nyingi hapa nchini zinatetereka mara baada ya aliyeanzisha kufariki au hali ya uchumi kubadilika kutokana na kukosa elimu ya biashara na kuitaka TRA kuangalia namna bora ya kuzitunza biashara kwa kuwaendeleza wafanyabiashara.
“Tuone namna ya kuwapatia elimu na kuwajengea misingi imara ya kuendeleza biashara zao ili ziweze kuwa endelevu na nchi isiwe inawapoteza wafanyabiashara mara kwa mara kutokana na biashara hizo kukosa misingi imara na kupoteza mapato ya Serikali” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi ameishauri TRA kuanzisha mfumo mzuri wa kutoa mashine za EFD na kuzitengeneza zinapoharibika na kuhakikisha wafanyabiashara wanakuwa nazo wakati wote ili kupunguza malalamiko ya wafanyabiashara, mianya ya rushwa na ukwepaji wa kodi za Serikali.
“Mashine za EFD ni muhimu kwa Serikali katika ukusanyaji wa mapato, ni wakati sasa TRA iweke mkakati wa kuhakikisha inachukua jukumu la kuhakikisha mashine hizi zinapatikana kiurahisi na kila mfanyabiashara anayetakiwa kuwa nayo anayo na ikiharibika inatengenezwa kwa wakati bila usumbufu” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, ameitaka TRA kutoa elimu ya kina kuhusu masuala ya kodi na umuhimu wake kwa Taifa na kutoa motisha kwa walipa kodi wa kati na wa chini ili kuwavutia watu wengi zaidi kulipa kodi kwa hiari kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Mhe. Mtambi ameiomba TRA kufuatilia ulipaji wa kodi katika migodi ya wachimbaji wa kati na wachimbaji wadogo wadogo ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu na kusaidia katika mkakati wa kuziba mianya yote ya utoroshaji wa madini hapa nchini.
Aidha, ameitaka TRA kudhibiti bidhaa za magendo na utoroshaji wa mifugo kutoka Mkoa wa Mara kwenda nchi jirani ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali, kusaidia Mkoa uweze kuanzisha na kukuza viwanda vya kuchakata nyama na kuzalisha ajira zaidi kwa ajili ya Watanzania.
Mhe. Mtambi amewapongeza watumishi wa TRA wanaofanya kazi katika Kituo cha Forodha Sirari kwa ujasiri wao wa kukabiliana na magendo na kumhakikishia Kamishna Jenerali wa TRA kuwa Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Mara itaendelea kuwapa ushirikiano katika kukabiliana na biashara za magendo katika mpaka huo.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda amesema malengo ya ziara yake ni kujitambulisha kwa viongozi mbalimbali na kuonana na wafanyabiashara na watumishi wa mamlaka hiyo.
Bwana Mwenda amesema TRA inampango wa kuimarisha makusanyo ya kodi kwa kuimarisha elimu ya mlipakodi kwa wafanyabiashara na kuimarisha Kitengo cha Kudhibiti Magendo ili wafanyabiashara wote walipe kodi za Serikali kiuhalali.
Bwana Mwenda ameongelea umuhimu wa Mikoa kuimarisha Kamati za Ushauri wa Kodi za Wilaya yaani District Tax Advisory Committees ili ziweze kufanya kazi zake kiufanisi na kutatua migogoro mingi ya kikod katika maeneo yao na TRA ipo tayari kwa ushirikiano katika utekelezaji wa suala hilo.
Bwana Mwenda amesema Mkoa wa Mara ni kati ya Mikoa mikubwa ya kukodi kutokana na shughuli za kiuchumi zilizoko katika Mkoa huu na mpaka wa Sirari ambao unaingiza na kutoa kutoka Tanzania kwenda nchi za Kenya na Uganda na kadhalika.
Mapokezi hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuhudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Dominicus Lusasi na baada ya mapokezi hayo Bwana Mwenda na Msafara wake wamefanya kikao na watumishi wa TRA na kutembelea Kituo cha Forodha Sirari, Wilaya ya Tarime.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa