Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 24 Juni, 2024 ameshiriki katika Baraza Maalum la Madiwani la kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kuipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo na makusanyo ya Halmashauri.
“Huu ni ushahidi tosha kuwa kuna mshikamano wa dhati katika kuimarisha mifumo ya mapato na matumizi na kusimamia utendaji wa Serikali kwa ujumla” amesema Mheshimiwa Mtambi na kulipongeza Baraza la Madwani kwa usimamizi mzuri wa Halmashauri.
Mhe. Mtambi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa ukusanyaji wa mapato ambapo hadi kufikia tarehe 30 Mei, 2024 Halmashauri hiyo ilifanikiwa kukusanya asilimia 97 ya fedha zote zilizopangwa kukusanywa katika mwaka wa fedha 2023/2024.
“Ni matumaini yangu kuwa katika muda uliobakia Halmashauri itakusanya kwa asilimia 100 na zaidi katika mapato yake ya ndani ili yasaidie katika kuboresha huduma za wananchi wa Wilaya ya Rorya” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameliagiza Baraza la Madiwani kuhakikisha Halmashauri inaandaa mpango kazi wa kujibu hoja zote za CAG na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Seriklai za Mitaa (LAAC) yaliyotolewa mwaka 2023 na kuchukua hatua kwa wote wanaosababisha hoja za ukaguzi.
Aidha, Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri ihakikishe watumishi na MAdiwani wanapata mafunzo kuhusu Mfumo wa Taifa wa Manunuzi (NEST) na sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2023 na kanuni zake ili manunuzi ya umma yafanyike kwa kufuata sheria.
Amelitaka Baraza la Madiwani kusimamia utoaji wa mikopo ya vikundi na urejeshaji wa mikopo kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na mikopo ya Serikali kwa mujibu wa taratibu.
Kanali Mtambi amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuratibu mafunzo ya mifumo ya kielektroniki ya Serikali kwa Wakaguzi wa Ndani wa Mkoa wa Mara ili kupata uelewa na kuwawezesha kukagua mifumo hiyo kulingana na taratibu zinazotakiwa.
Mhe. Mtambi ameitaka Menejimenti ya Halmashauri hiyo kuandaa mpango mkakati wa kurejesha fedha zote zilizokopwa kwenye akaunti ya amana
Kanali Mtambi amelitaka Baraza la madiwani kusimamia ulipaji mkopo wa madiwani katika benki za NMB na CRDB, mkopo wa shilingi bilioni moja uliochukuliwa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kuhakikisha watumishi wote waliosababisha hoja za ukaguzi wanachukuliwa hatua za kiutumishi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mhe. Gerald Ng’ong’a amesema tangu madiwani hao walipoingia madarakani Halmashauri hiyo imeimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa sasa inafanya vizuri.
Katika ukaguzi huo, Halmashauri ilipata hoja 92 na maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) matano na hadi kufikia tarehe 24 Juni, 2024 hoja 38 zilikuwa zimejibiwa na kufungwa, hoja 54 utekelezaji wake unaendelea.
Mhe. Ng’ong’a ameahidi kuwa Halmashauri yake itatekeleza maagizo yote yaliyotolewa katika kikao hicho kwa wakati na kuahidi kuwa Baraza la Madiwani na wataalamu kuendelea kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Wilaya ya Rorya.
Mhe. Ng’ong’a ameeleza kuwa kwa sasa Halmashauri hiyo imeweka mkakati wa kupunguza madeni ya zamani kwa kujitahidi kukusanya mapato ya ndani ya kutosha ili kuyatumia kulipa madeni yake kila wakati.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya, wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Menejimenti na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa