Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 27 Juni, 2024 amefanya ziara katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na kuipongeza Halmashauri hiyo kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Ninawapongeza sana kwa usimamizi wa miradi na ubora wa majengo mnayojenga, hapa kazi inaonekana, mmepata mafundi wazuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kutunza taarifa za mafundi wake wanaofanya kazi vizuri ili mafundi hao waweze kutumika katika kutekeleza miradi mingine itakayokuja katika Halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ametembelea na kukagua mzani wa ukaguzi wa magari wa Robana uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda na kujionea namna mzani huo unaopima magari yakiwa kwenye mwendo unavyofanya kazi.
Akiwa katika mradi huo, Mkuu wa Mkoa ametaarifiwa kuwa mradi umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake na kwa sasa mzani huo umeanza kufanyakazi na kupunguza msongamano wa magari katika mzani wa awali uliokuwepo katika eneo hilo.
Baada ya hapo, Mhe. Mtambi ametembelea Shule ya Sekondari ya Migungani inayoendelea kujengwa katika eneo hilo na kukagua mradi wa vyumba sita vya madarasa na matundu nane ya vyoo unaoendelea kutekelezwa katika eneo hilo.
Akiwa katika shule hiyo, Mkuu wa Mkoa mbali na kukagua ujenzi, amesalimiana na wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne wanaoendelea kujisomea katika shule hiyo na kuzungumza na baadhi ya walimu wa shule hiyo waliokuwepo katika eneo la shule.
Baada ya hapo, Mhe. Mtambi ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda na kupongeza kuanza kwa utoaji wa huduma katika Hospitali hiyo na kuitaka Halmashauri hiyo kutumia mapato ya ndani kukamilisha majengo ambayo hayajakamilika katika hospitali hiyo.
Mkuu wa Mkoa pia alifanya mkutano na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda na kuwakumbusha watumishi kuhusu uadilifu na kuwataka kurudi kwenye misingi ya utumishi wa umma katika kuwatumikia wananchi.
Mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara yake kwa kushiriki kikao cha Baraza la Madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vincent Anney Naano amewapongeza wasimamizi wa ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo.
Mhe. Dkt. Naano amesema mradi huo utakapokamilika utaiwezesha Serikali kutoa huduma za Hospitali ya Mji kwenye hospitali yake badala ya kuendelea kuitumia Hospitali Teule ya Halmashauri ya Mji wa Bunda (DDH) inayomilikiwa na taasisi za kidini iliyopo katika Mji wa Bunda.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Bunda, wakuu wa taasisi za umma, maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na wasimamizi wa miradi iliyotembelewa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa