Mkuu wa Mkoa wa Mara leo tarehe 26 Juni, 2024 ameshiriki kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi ya ukaguzi na ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Mtambi amesema Halmashauri hiyo imepata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo jambo ambalo linaonyesha kuwa kuna kazi kubwa inafanyika katika halmashauri hiyo na ushirikiano kati ya viongozi na watendaji.
“Ninaipongeza Halmashuri kwa kufanikiwa kukusanya shilingi 1,765,822,401 hadi kufikia tarehe 3o Mei, 2024 ambayo ni sawa na asilimia 90.2 ya makusanyo ya shilingi 1,955,676 yaliyopangwa kukusanywa kwa mwaka wa fedha 2022/2023” amesema Mhe. Mtambi.
Aidha, Mhe. Mtaambi amesema amepata taarifa kuwa hadi kufikia tarehe 25 Juni, 2024 Halmashauri hiyo imefikia asilimia 96 ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Mhe. Mtambi ametoa siku saba kwa Halmashauri za Mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuwa zimekamilisha mchakato wa kugawana mali na madeni yaliyotokana na iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kabla ya kuanzishwa kwa Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Mhe. Mtambi ameitaka RUWASA kuhakikisha Mji wa Kibara unapata maji safi na salama ya uhakika kwa kuandaa mradi mkubwa wa kusambaza maji katika eneo hilo na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Bunda kufuatilia kwa karibu.
Kanali Mtambi amewataka Madiwani kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji kuhamasisha chakula cha watoto mashuleni na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ya utawala.
Katika taarifa ya ukaguzi wa CAG, Halmashauri ilipata hoja 78 maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za (LAAC) 15 kwa kipindi cha kuanzia 2012/2013 hadi 2022/2023, hoja 17 kwenye mfuko wa pamoja wa afya, hoja 9 za mfuko wa vijana na watu wenye ulemavu .
Taarifa hiyo imeonyesha kuwa hoja za nyuma zilikuwa 54 na kati ya hizo hoja mbili zimefungwa,hoja tisa zinaendelea na utekelezaji haujaanza. Imepata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Charles Manumbu amesema Halmashauri ilianza mwaka 2016, madiwani waliopo kwa sasa wameanza 2020 na kwa wakati huo kulikuwa na malalamiko mengi sana.
“Tulisimama kwenye Sheria, kanuni na taratibu na kuchukua hatua mbalimbali za kurekebisha hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuwaondoa baadhi ya watumishi waliokuwa hawana mwenendo mzuri na kwa sasa Halmashauri yetu imetulia” amesema Mhe. Manumbu.
Mhe.Manumbu amesema kwa sasa Halmashauri ina miradi mingi ambayo haikamiliki nakutokana na jiografia ya Halmashauri kukaa vibaya, gharama kubwa inatumika kwenye usafiri kwa watendaji kwenda kusimamia miradi, kukagua na kutoa huduma kwa wananchi.
“Katika ukusanyaji wa mapato tangu Halmashauri ilipoanza haikuwahi kukusanya mapato kufikia asilimia 90 lakini mwaka huu hadi kufikia sasa tayari Halmashauri imefikia asilimia 96 ya ukusanyaji wa mapato yaliyopangwa kukusanywa mwaka 2023/2024.
Mhe. Manumbu amesema anategemea kuwa mwaka huu Halmashauri hiyo inaweza kufikia asilimia 100 au zaidi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mara ya kwanza katika historia.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa