Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Mtambi leo ameongoza ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kilele cha Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara yaliyofanyika katika Mji wa Sekanani, Narok, Nchini Kenya na kuwataka wadau kushirikiana kulinda ikolojia ya bonde la Mto Mara.
“Kutokana na umuhimu wa bonde la Mto Mara kwa wananchi, wanyama na shughuli za utalii katika hifadhi zetu za Maasai Mara na Serengeti ni muhimu wadau wote kushirikiana na kulilinda bonde hilo kwa nguvu zetu zote” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema tafiti mbalimbali zimefanyika katika bonde la Mto Mara na kuwataka wataalamu kuhakikisha kuwa tafiti hizo zinatumika kuboresha utunzaji wa mazingira katika bonde la Mto Mara kwa manufaa mapana ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni wa wananchi wanaoishi katika eneo hilo.
Mhe. Mtambi ambaye amemwakilisha Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, amesema Sera ya Taifa ya Maji ya Tanzania ya mwaka 2022 na Sheria ya Menejimenti ya Rasilimali za Maji zinawahimiza wananchi, taasisi na wadau wote kutunza vyanzo vya maji kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Mhe. Mtambi ameipongeza Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) na kamati ya maandalizi kwa kufanikisha maandalizi ya maadhimisho hayo na kuwakaribisha wadau wote katika maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mara ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 12 Septemba, 2025 katika eneo litakalopangwa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) Dkt. Masinde Bwire amesema uhifadhi wa bonde la Mto Mara ni muhimu sana kwa kuwa ni maliasili ya ulimwengu mzima na tunawajibika kuitunza kwa maendeleo maendeleo ya wananchi, wanyama na uhifadhi wa ikolojia kwa maendeleo endelevu.
Dkt. Bwire amezitaka Serikali za Tanzania na Kenya kutenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na upandaji wa miti katika bonde la Mto Mara ili kuilinda ikolojia ya eneo hilo kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Dkt. Bwire amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira ya bonde la Mto Mara na kuwasikiliza wataalamu na watafiti wanavyoshauri kuhusu namna bora ya kuendelea kuhifadhi mazingira ili kuendelea kupata manufaa ya uhifadhi na ikolojia katika bonde hilo.
Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza wafadhili wa Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara ambao wamewezesha shughuli mbalimbali za maadhimisho hayo kuanzia tarehe 12 Septemba, 2024 hadi leo siku ya kilele cha maadhimisho hayo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kenya Bwana Abdi Dubat amesema Bonde la Mto Mara liko katika hatari ya kuharibiwa ikolojia yake kutokana na ukataji wa miti, shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi.
Bwana Dubat ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amesema ili kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Kenya ina mpango wa kupanda miti bilioni 15 katika kipindi cha miaka kumi katika nchi hiyo na Bonde la Mto Mara limepewa kipaumbele kwa ajili ya kupanda miti huo kutokana na umuhimu wake.
Bwana Dubat amewapongeza wananchi wa Narok pamoja na viongozi kwa shughuli za utunzaji wa mazingira wanazozifanya na kuwataka waendelee kwani ni muhimu wa wanyama, vyanzo vya maji na shughuli za utalii endelevu katika eneo hilo.
Bwana Dubat amewataka wageni wote kutembelea vivutio vya utalii mbalimbali vilivopo Narok na hususan Hifadhi ya Maasai Mara iliyopo katika eneo hilo.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya 13 ya Siku ya Mara ni Kwa Pamoja: Tuhifadhi Bonde la Mto Mara kwa Bioanuai Endelevu na Ustahimilivu wa Tabia nchi” yaani “Flowing Forward Together: Conserving the Mara Basin Ecosystem for Sustainable Biodiversity and Climate Resilience.”
Maadhimisho haya yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Tanzania ikiwemo maafisa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, viongozi na baadhi ya maafisa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Mkoa wa Mara.
Wengine waliohudhuria ni wafanyabiashara, taasisi zinazohusika na uhifadhi, wadau, Waandishi wa Habari na vikundi vya utamaduni kutoka Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa