Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo tarehe 18 Septemba, 2024 amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na kuzungumza na wananchi, kutembelea migodi ya Polly Gold na Seka iliyopo katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Mtambi amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kigera Etuma na kutoa saa 48 kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma kutoa taarifa za mahali alipo mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kigera anayedaiwa kutoroshwa na mwanaume wa kijijini hapo huku aliyemtorosha akipata dhamana.
Mhe. Mtambi ametoa maagizo hayo baada ya Mama mzazi wa mwanafunzi huyo kudai kuwa mtuhumiwa ambaye mara ya mwisho alikuwa na mtoto wake ameachiwa na yupo kijijini hapo wakati yeye hajui mtoto wake alipo.
Kanali Mtambi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Musoma kufuatilia wazazi na walezi wa wanafunzi watano waliopewa mimba katika Shule ya Sekondari Kigera na ambao watuhumiwa hawajakamatwa au walikamatwa na kuachiwa na baadaye kutoroka.
Aidha, Mhe. Mtambi amewahamasisha wananchi wa Kijiji hicho kuacha kufanya starehe kwa kuweka mziki mara kwa mara na kuacha kuzingatia usalama awa watoto wao baada ya baadhi ya wananchi kulalamikia Maafisa Utamaduni kutoa vibali vya muziki mara kwa mara kwa ajili ya watu kupiga muziki katika eneo hilo.
Mhe. Mtambi pia amewataka viongozi na wananchi wa eneo hilo kuhakikisha kuwa miradi ya kuihudumia jamii (CSR) inayotolewa na wamiliki wa migodi ya dhahabu katika eneo hilo inakuwa miradi endelevu itakayochechemua maeneo ya kijiji hicho.
Mhe. Mtambi amesema hamna maana kama wawekezaji hao watapatiwa miradi midogo midogo ambayo inaweza kufanyika kwa michango ya wananchi na ambayo haina tija kwa maendeleo endelevu ya kijiji hicho na wananchi wake, badala yake wawekezaji hao wapewe miradi ya kimkakati itakayokuza uchumi wao.
Mhe. Mtambi amewaagiza wawekezaji katika migodi ya madini katika eneo hilo kupunguza vumbi barabarani kwa kumwagia maji wakati wanaposafirisha mawe yenye dhahabu ili kulinda afya za wananchi wa kijiji hicho na miundombinu ya barabara.
Akiwa katika mkutano huo, Mhe. Mtambi amewahamasisha wazazi kuchangia chakula cha watoto shuleni baada ya wananchi kushuhudia wanafunzi ambao hawana chakula wakiwa wanawaangalia wanafunzi wengine ambao walikuwa wanakula wakati wa mapumziko ya mchana katika Shule ya Msingi Kigera.
Baada ya mkutano huo, Mhe.Mtambi ameitebelea migodi ya Polly Gold na Seka na kujionea namna uzalishaji unavyofanyika na kujadiliana na migodi hiyo kuhusiana na namna bora ya kupunguza vumbi katika vijiji vinavyopitiwa na magari ya migodi hiyo.
Aidha, ameitaka migodi hiyo kutoa ajira kwa wananchi wanaoizunguka migodi hiyo ili kujenga uhusiano endelevu na wananchi hao.
Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma, baadhi ya watumishi kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na viongozi wa migodi hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa