Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ofisini kwake amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa waandamizi kutoka Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) waliopo katika Mkoa wa Mara kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha wadau wa usafiri wa majini kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kinachotarajiwa kufanyika Novemba, 2024.
Akizungumza na maafisa hao, Mhe. Mtambi ameipongeza TASAC kwa hatua mbalimbali wanazochukua kuimarisha usafiri wa majini na ushirikiano wanaoutoa katika Mkoa wa Mara na hususan usalama wa wasafiri katika katika Ziwa Victoria.
“Sisi kama Serikali tunatakiwa kuendelea kuwahakikishia usalama watumiaji wa Ziwa Victoria ikiwemo wasafiri wanaotumia vyombo vya usafiri vya majini kuhusiana na usalama wao wanapotumia usafiri wa majini” amesema Mhe. Mtambi.
Kanali Mtambi ameiomba TASAC kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria na kanuni zinazohusiana na usafiri wa majini kwa wananchi na taasisi za Serikali na binafsi ili kupunguza ajali na athari za ajali za vyombo vya usafiri wa majini.
Mhe. Mtambi ametumia nafasi hiyo kupendekeza kuwa kikao cha wadau wa TASAC Kanda ya Ziwa kifanyike katika Mkoa wa Mara ambao una asilimia 38 ya Ziwa Victoria katika Wilaya za Bunda, Musoma, Butiama na Rorya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira na Usafiri wa Majini Bi. Leticia Mutaki amesema lengo la kikao hicho cha wadau ni kuweka mikakati ya pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujilinda na kujiokoa ajali zinapotokea.
Bi. Mutaki amesema TASAC inaendelea na jukumu lake la utoaji wa elimu ya usalama wa usafiri majini kwa wadau wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo taasisi na Halmashauri kuhusiana na usimamizi wa usafiri wa majini.
“Tuna mpango wa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Halmashauri zote zinazopakana na ziwa ili Halmashauri zisaidie kusimamia usafiri wa majini kwa niaba ya TASAC” amesema Bi. Mutaki.
Bi. Mutaki amesema kwa sasa ujenzi wa Kituo cha Utaftaji na Uokoaji cha Mwanza yaani Maritime Rescue Coordination Centre (MRCC) katika Ziwa Victoria kimekamilika na ambacho kinatarajiwa kusaidia katika kupunguza madhara ya ajali na zoezi la uokoaji katika Ziwa Victoria wakati ujenzi wa kituo kama hicho katika Manispaa ya Musoma unaendelea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TASAC Bi. Judith Kakongwe amesema Sheria na kanuni za sasa zinawabana zaidi wenye vyombo vya usafiri kuweka life jackets lakini haziwabani abiria kuzivaa jambo ambalo linaleta changamoto kwa sababu wamiliki wakiweka bila kuvaliwa hazisaidii kama inatokea ajali.
“Tupo kwenye mchakato wa kubadili vipengele vya sheria na kanuni ili abiria nao wabanwe kuvaa life jackets na sio tu wamiliki wa chombo kama ilivyo sasa ili kusaidia kupunguza madhara ajali zinapotokea” amesema Bi. Kakongwe.
Katika ziara hiyo viongozi hao wa TASAC wameambatana pia na Meneja Uhusiano na Masoko Bwana Said Mkabakuli.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa