Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo ameshiriki kikao maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na kuiagiza Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA) kupeleka maji bure Shule ya Msingi Nyamikoma B iliyopo katika eneo la Pida, Wilaya ya Butiama.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo baada ya wananchi kuwasilisha malalamiko kuhusu RUWASA kukitumia kisima cha shule hiyo kilichochimbwa kwa ufadhili wa Shirika la PCI shuleni hapo na kuyasambaza katika eneo hilo na kuidai shule hiyo kulipa bili za maji kama watu na taasisi zilizopo katika eneo hilo.
“Naagiza maji kwenye shule hii yaletwe haraka na watatumia bure kwa sababu kisima hiki ni cha kwao kilichimbwa na mfadhili wao ili watoto waweze kupata maji kiurahisi, hamna kuwaletea bili za maji” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi ameagiza kuwa kwa kuwa shule hiyo imetoa kisima chake bure na kuruhusu maji yake yasambazwe kwa wananchi wa maoneo hayo, RUWASA itumie busara kurudisha huduma za maji katika shule hiyo haraka iwezekanavyo.
Mhe. Mtambi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Butiama kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kufuatilia pampu zilizokuwa zimefungwa katika kisima hicho ambazo RUWASA wanadai waliikabidhi kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo na Mwalimu Mkuu anadai ipo RUWASA.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Bibi Eunice Makere ameeleza kuwa alipokea malalamiko hayo kutoka katika shule hiyo na kufanya kikao na RUWASA, uongozi wa Kijiji na uongozi wa watumia maji na kubaliana maji hayo yarejeshwe kabla shule hazijafunguliwa.
Bibi Makere amesema hata hivyo baada ya maji hayo kuunganishwa katika tanki lililojengwa na RUWASA na shule kutakiwa kulipia maji wanayoyatumia, shule hiyo haijaweza kulipia maji hayo na wanafunzi wa shule hiyo wamekosa maji kutokana na maamuzi hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Butiama Mhe. Christopher Marwa Siagi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa michango yake aliyoitoa katika Baraza hilo maalum inayolenga kuleta tija.
Mhe. Siagi amemuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia Shule ya Sekondari ya Mkono iliyopo katika Wilaya ya Butiama kupata maji kutokana na shule hiyo kuwa na wanafunzi wengi na kukosa maji ya uhakika ya kutumia.
Aidha, Mhe. Siagi ameitaka Halmashauri hiyo kutoa taarifa za fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo pindi fedha zinapoingia ili kukiwezesha Chama cha Mapinduzi kufanya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa kutokana na fedha hizo.
Kikao cha Baraza la Madiwani kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Hamashauri ya Wilaya ya Butiama.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa