Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela amewataka wakandarasi waliopata zabuni za kutekeleza miradi ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) katika Mkoa wa Mara kukamilisha ujenzi wa barabara hizo kwa wakati.
Bwana Msovela ametoa maagizo hayo leo tarehe 30 Julai 2021 katika hafla ya kusaini mikataba na wakandarasi 122 waliopewa zabuni za kutengeneza barabara, vivuko na madaraja katika wilaya zote za Mkoa wa Mara.
“Niwaombe wakandarasi tujitahidi kukamilisha barabara hizi kwa wakati ili wananchi waweze kupata urahisi wa kusafiri na kusafirisha mizigo yao ikiwemo mazao yao kwa wakati” alisema Bwana Msovela.
Aidha amewataka wakandarasi kulipa tozo zozote za kisheria kwa halmashauri na mamlaka nyingine za serikali kwa wakati ili waweze kuendelea kufanya kazi zao vizuri bila kusmbuliwa.
Katibu Tawala pia amewakumbusha wakandarasi kutekeleza matakwa ya sheria za mazingira wakati wa ujenzi wa barabara hizo ili kuleta maendeleo endelevu ya Mkoa wa Mara.
Bwana Msovela amewaagiza wakandarasi hao kuajiri vibarua katika kazi za ujenzi kwenye miradi huo kutoka maeneo wanayojenga barabara hizo ili wananchi waweze kupata ajira na serikali ipate walinzi wa barabara zake.
Ameitaka TARURA kuimarisha usimamizi na kuhakikisha kuwa barabara hizo zinakamilika kwa wakati, kwa viwango vilivyokubalika na ubora unaoridhisha kwa mujibu wa mikataba.
“Mkisimamia kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni barabara hizi zitakamilika kwa ubora na katika muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba” alisema Bwana Msovela.
Bwana Msovela ameziomba taasisi za fedha kuongeza ushirikiano wa kibiashara na wakandarasi hao ili barabara za Mkoa wa Mara ziweze kukamilika kwa wakati.
Ameelezea matumaini yake kuwa baada ya kukamilika kwa barabara hizi zitaenda kuufungua Mkoa wa Mara kimawasiliano na kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Kwa upande wake akizungumza katika ufunguzi wa hafla hiyo Mratibu wa TARURA Mkoa wa Mara Mhandisi Musa Z. Mzimbiri ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kujenga barabara, vivuko na madaraja katika Mkoa wa Mara.
“Serikali pia imetenga zaidi shilingi bilioni 13.4 kwa ajili ya barabara za majimbo 10 ya uchaguzi ya Mkoa wa Mara katika kutekeleza miradi ya barabara za majimbo ya uchaguzi” amesema Mhandisi Mzimbiri.
Mhandisi Mzimbiri ameeleza kuwa miradi ambayo imewekwa saini leo ni miradi 122 inayotekelezwa na wazabuni 34 yenye gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 6.044 katika halmashauri na wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Hafla fupi ya kutia saini ya ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA ilihudhuriwa pia na viongozi wa taasisi za kifedha, bima, madini, wakandarasi, maafisa kutoka Ofisi ya Mratibu wa TARURA Mkoa wa Mara na waandishi wa habari.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa