Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela leo tarehe 4 Novemba, 2021 amekagua miundombinu ya elimu inayojengwa kwa kutumia fedha za kupambana na UVIKO 19 katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Bwana Msovela amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mara kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo inakamilika kabla ya Desemba 1, 2021 ili kuruhusu wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza shule mapema.
“Kama alivyoelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi, miundombinu hii inatakiwa ikamilike kabla ya Desemba 1, 2021 kuruhusu wanafunzi kuanza masomo yao ifikapo Januari, 2021 bila kuchelewa”.
Aidha Bwana Msovela amezitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa thamani ya fedha yaani value for money inaonekana katika ujenzi wa miradi hii.
Bwana Msovela ameeleza kuwa pamoja na miradi hiyo kujengwa ndani ya muda mfupi, amezitaka Halmashauri kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotakiwa katika ujenzi huo.
Mkoa wa Mara umepokea shilingi 2, 380, 000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Shule za Sekondari na shilingi 1,923,744,759.72 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika Shule Shikizi za Msingi.
Katika fedha zilizopokelewa katika Mkoa wa Mara, Halmashauri ya Wilaya ya Butiama imepokea shilingi 1,440,000,000.00 kwa ajili ya shule za sekondari na shilingi 200,000,000 kwa ajili ya kujenga madarasa katika Shule Shikizi za Msingi.
Ujenzi wa miundombinu za elimu katika Mkoa wa Mara umeanza katika Halmashauri zote na upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa