Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela ameipongeza Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma kwa kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa kuanzia mwaka 2020.
Bwana Msovela ametoa pongezi hizo leo tarehe 2 Septemba wakati alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi katika hafla ya kutoa tuzo kwa wanafunzi na walimu waliofanya vizuri katika mitihani mbalimbali.
“Ninawapongeza sana kwa kuongeza taaluma hususan katika mitihani ya kidato cha sita, hata hivyo mwaka 2022 shule hii ilenge kuwa kwenye kumi bora kitaifa, inawezekana” alisema Bwana Msovela.
Bwana Msovela amewataka walimu na wanafunzi wa shule hiyo kuongeza juhudi katika kujifunza na kufundisha ili kuweza kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ijayo.
Bwana Msovela amewataka wanafunzi kuzingatia masomo na kuwa na nidhamu kwa walimu wanaowafundisha ili kuweza kufanikiwa katika masomo yao.
“Ninaipongeza Bodi ya Shule kwa kuona umuhimu wa kuwapa motisha walimu ambayo ni muhimu sana katika kupandisha ari ya walimu kufundisha na kuwasimamia wanafunzi katika masomo yao” alisema Msovela.
Aidha amewataka viongozi na wasimamizi wa sekta ya elimu kusikiliza changamoto za walimu na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka ili kuwapa nafasi walimu kutumia muda wao katika kuwasaidia wanafunzi katika masomo yao.
Awali akitoa taarifa kwa Katibu Tawala, Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Mohamedi Kajeri ameeleza kuwa katika miaka ya 2020 na 2021 ufaulu katika mitihani ya kitaifa unaongezeka kutokana na juhudi za walimu na wanafunzi.
“Katika mwaka 2020 matokeo ya ujumla ya shule hii katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne shule ilikuwa katika nafasi ya 436 kati ya shule 3,908 kitaifa wakati mwaka 2020 shule imekuwa ya 205 kati ya shule 3,956” alisema Mwalimu Kajeri.
Mwalimu Kajeri ameeleza kuwa ameeleza katika matokeo hayo wanafunzi waliopata daraja la kwanza walikuwa 52, daraja la pili 27, daraja la tatu 14, daraja la nne 8 na daraja la sifuri 5 ambalo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100.
Aidha Mwalimu Kajeri ameeleza kuwa katika mtihani wa kidato cha sita Mwaka 2019 ilikuwa nafasi ya 477 kati ya shule 594, mwaka 2020 shule ilikuwa ya 490 kati ya shule 586 wakati mwaka 2021 shule ilifanya vizuri na kufanikiwa kuwa shule ya 101 kati ya shule 610.
Mwalimu Kajeri ameeleza kuwa katika hafla hiyo shule imetoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya ndani na kitaifa na walimu pamoja na watafsiri lugha za alama kwa mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili, nne, na sita kwa mwaka 2020/2021.
“Katika hafla hii, shule imetoa zawadi zenye jumla ya shilingi 8,700,000 kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya mtotisha kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri” alisema Mwalimu Kajeri.
Shule ya Sekondari ya Musoma Ufundi ni shule ya serikali ya wavulana ya bweni yenye wanafunzi 983 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na ilianzishwa mwaka 1959 wakati huo ikijulikana kama Musoma Alliance.
Mwalimu Kajeri ameeleza kuwa shule ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne 510 na wanafunzi wa kidato cha tano na sita 473 ambao wanasoma katika michepuo ya PCM, CBG, EGM, HGE, HGK, HGL na PGM.
Ameeleza kuwa shule hii pia inachukua wanafunzi wenye ulemavu na kwa sasa shule ina jumla ya wanafunzi 104 wenye ulemavu wa kutosikia, kuongea, Ngozi, viungo na usonji.
Mwalimu Kajeri ameeleza kuwa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma ina walimu 71 na watumishi wasio walimu wanne walioajiriwa na 11 wanye ajira za mkataba.
Hafla ya utoaji wa tuzo kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri imehudhuriwa pia na bodi ya shule hiyo, Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Musoma, Bodi ya Shule, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa