MSOVELA AFANYA UKAGUZI WILAYA TATU
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela leo tarehe 6 Novemba 2021 ameendelea na ukaguzi wa miradi kwa kufanya ukaguzi katika Wilaya nne wa ofisi za Maafisa Tarafa na pamoja na miradi miundombinu inayoendelea kujengwa kutokana na fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Akizungumza katika maeneo mbalimbali Bwana Msovela amewakumbusha wasimamizi wa miradi kuwa Mkoa wa Mara umeazimia kukamilisha miradi hiyo tarehe 1 Desemba 2021 ili kuruhusu wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo kwa wakati.
“Kama Mkuu wa Mkoa alivyoagiza, miradi hii tunapaswa kuikamilisha kabla ya muda uliopangwa na serikali,na hili tukiongeza juhudi inawezekana lengo hilo likatimia kwa wakati” alisema Bwana Msovela.
Katika miundombinu inayojengwa, Bwana Msovela ameshuhudia miundombinu ikiwa katika hatua mbalimbali za kujenga msingi na kuwataka Wasimamizi wa Kata kutoka Halmashauri kwenda kusimamia kwa ukaribu miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati kama ilivyopangwa.
Aidha kutokana na uchakavu wa Ofisi za Maafisa Tarafa, Bwana Msovela aliagiza kuwa fedha za ukarabati wa majengo hayo zitengwe katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ili yaweze kukarabatiwa.
Aidha alisema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara itaangalia uwezekano wa kununua samani za ofisi na vitendea kazi kwa ajili ya Maafisa Tarafa wa Mkoa mzima.
Katika ziara hiyo, Bwana Msovela alikagua Ofisi ya Afisa Tarafa ya Suba, Shule ya Sekondari ya Suba, Shule ya Sekondari ya Buturi, Shule ya Sekondari ya Pasta Raphael Odunga na Ofisi ya Afisa Tarafa Luo Imbo katika Wilaya ya Rorya.
Katika Wilaya ya Tarime alikagua Ofisi ya Afisa Tarafa ya Inano na Ofisi ya Afisa Tarafa ya Inchage. Katika Wilaya ya Serengeti Katibu Tawala alitembelea Ofisi ya Afisa Tarafa ya Ikorongo, nyumba iliyojengwa kwa ajili ya Afisa Tarafa ambayo haijapokelewa na Serikali baada ya kujengwa chini ya kiwango, Kituo cha Afya Kenyana na Shule ya Sekondari ya Samoche.
Katika Wilaya ya Butiama, Katibu Tawala alitembelea Ofisi na nyumba ya kuishi Afisa Tarafa ya Kiagata, Shule ya Sekondari ya Bumangi na Ofisi ya Afisa Tarafa ya Makongoro.
Bwana Msovela aliambatana na Kaimu Mhasibu Mkuu wa Mkoa Bwana Pascal Kajuna, Mkaguzi Mkuu wa Ndani Bwana Yusuf Luhende, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi- Miundombinu Mhandisi Richard Moshi, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi- Utawala na Rasilimaliwatu Bwana Dominicus Lusasi na Mwakilishi wa Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara Bwana Fidel Baragaye.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara za Katibu Tawala kukagua miradi Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa