Mratibu wa Mradi wa BOOST, Mkoa wa Mara Mwl. Adam Janga leo ametoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST kwa maafisa kutoka Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Dunia ambao wameanza ziara ya ukaguzi wa mradi huo katika Mkoa wa Mara.
Mwl. Janga ameyataja mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la uandikishaji wa elimu ya awali ambapo hadi kufikia tarehe 07 Machi, 2024, jumla ya wanafunzi 84,490 walikuwa wameandikishwa kutoka katika maoteo ya awali ya kuandikisha wanafunzi 82,679 ambayo ni sawa na asilimia 102.19.
“Baada ya maboresho ya miundombinu ya elimu katika shule za msingi, Mara tumeshuhudia angezeko hili ambalo ni sawa na asilimia 2.19 ikiwa ni sawa a ongezeko la wanafunzi 1,811 walioongezeka na kuvuka lengo la uandikishaji kwa mwaka 2024” amesema Mwl. Janga.
Bwana Janga ameeleza kuwa katika afua ya ujenzi wa miundombinu, mradi umetoa shilingi bilioni 12.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 17, vyumba vya madarasa 113 kwenye shule za zamani 52, vyumba vya madarasa ya mfano ya elimu ya awali 18, vyumba vya madarasa ya elimu maalum viwili, matundu ya vyoo 144 na nyumba moja ya walimu (two in one) katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
“Miradi yote ya ujenzi imekamilika na inatumika, shule mpya zimesajiriwa na zimeanza kuchukua wanafunzi na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za awali” amesema Bwana Janga.
Katika afua ya shule salama, mamlaka za Serikali za Mitaa zimetekeleza afua hii katika shule 523 kwa kuhamasisha jamii kuhsu mpango salama wa wanafunzi, vikao na midahalo ya wanafunzi, dawati la Jinsia, vikao vya Baraza la Watoto, kuanzisha masanduku ya kupokea maoni, na kuteua walimu wa unasihi katika Shule zote za msingi katika Mkoa wa Mara.
Mwalimu Janga ameeleza kuwa katika utekelezaji wa afua ya njia bora na matumizi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika madarasa ya elimu ya awali, shule za msingi 140 za Mkoa wa Mara zimepokea vitabu vya hadithi za watoto wa elimu ya awali na kusaidia kupunguza wanafunzi wasiomudu KKK katika shule za awali na msingi.
Katika afua ya MEWAKA, Mwalimu Janga ameeleza kuwa kwa sasa shule zote za msingi 835 za Mkoa wa Mara zinatekeleza mpango huu na makakati wa Mkoa ni kuwajengea uwezo viongozi na wadau wa elimu kuhusu usimamizi wa shughuli za MEWAKA na kuendelea kusimamia na kuimarisha jumuiya za kujifunzia na kuboresha uwezo wa walimu katika ufundishaji na ujifunzaji.
Mwal. Janga amesema katika afua ya shule za msingi na vituo vya walimu kutekeleza mtaala wa TEHAMA, shule teule na vituo vya walimu vimefanya mafunzo ya TEHAMA, jumla ya shule teule tisa zimepokea vifaa vya TEHAMA na kuwafanya walimu kuanza kufundisha kwa kutumia TEHAMA.
“Ufundishaji kwa njia ya TEHAMA umeongeza ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kumaliza shule ya msingi mwaka 2023 ambapo ufaulu ulikuwa ni asilimia 76.04 ambao umepanda kwa asilimia 1.51 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo ufaulu ulikuwa ni asilimia 74.53” amesema Mwl. Janga.
Katika suala la kutenga bajeti ya shughuli muhimu za mradi, Mwal. Janga ameeleza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zilikumbushwa kuhusu kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mahitaji mbalimbali ya elimu ya awali na msingi na kwa sasa Halmasahuri za Mkoa wa Mara zinaendelea kutenga na kutekeleza bajeti kwa ajili ya masuala ya elimu ya msingi.
Katika utekelezaji wa afua ya utawala bora katika elimu na uongozi wa shule, Mwal. Janga ameeleza kuwa Mkoa wa Mara umewapatia mafunzo walimu wakuu wote 835 wa Shule za Msingi kupitia mradi wa BOOST yaliyowezeshwa na wakufunzi kutoka Wakala wa Maendeleo ya Elimu Tanzania (ADEM) tarehe 02-07 Oktoba, 2023.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu amesema utekelezaji wa mradi huu kwa Mkoa wa Mara umekuwa shirikishi na unawahusisha maafisa kutoka Sehemu na Vitengo mbalimbali.
Aidha, Bwana Masatu ameeleza kuwa Mradi wa BOOST umekuwa ni moja ya ajenda za kudumu katika vikao mbalimbali vya menejimenti, Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na Mkoa uliunda kundi sogozi (whatsap group) ambapo taarifa zote za ujenzi zilikuwa zinawafikia viongozi wote wa Mkoa wa Mara kila wiki.
Dkt. Masatu amewakaribisha maafisa hao na kuwahakikishia uongozi wa Mkoa wa Mara utakuwa tayari muda wote kupokea maelekezo yoyote kuhusu uboreshaji wa utekelezaji wa mradi huo na elimu ya msingi kwa ujumla.
Aidha amewataka maafisa hao kutumia fursa ya kuwepo Mkoa wa Mara kutembelea vivutio mbalimbali vilivyomo ikiwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, fukwe za Ziwa Victoria na nyumbani na Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama. Mwal.
Mkoa wa Mara ni miungoni mwa mikoa 26 inayotekeleza Mradi wa BOOST ambao ni sehemu ya Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) ambao umekusudia kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi Tanzania Bara kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2026.
Katika mapokezi hayo, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Ayoub Mbilinyi, wajumbe wa Mradi wa BOOST Mkoa wa Mara na baadhi ya maafisa kutoka Sehemu ya Elimu pia walihudhuria kikao hicho.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa