Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) leo ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mara ambapo amefanya ziara katika Wilaya ya Bunda na kuzungumzia mpango wa Serikali kuwa na shule ya msingi kila kijiji.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua Shule ya Msingi Kihumbu, Mhe. Majaliwa amesema Serikali inampango pia wa kujenga Shule za Msingi katika vitongoji vyenye watoto wengi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hizo.
Mhe. Majaliwa amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Kihumbu kwa kutoa eneo lao bure kwa ajili ya mradu wa ujenzi wa Shule ya Msingi Sabasita na kushiriki katika kusafisha eneo hilo kabla ya ujenzi wa shule hiyo kuanza.
Akizungumza baada ya kukagua, kutembelea na kupanda mti wa kumbukumbu katika shule hiyo, Mhe. Majaliwa amewataka wananchi kuendelea kutoa michango ya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, nyumba za walimu, vyoo na kadhalika yenye kibali cha Mkuu wa Wilaya.
Mhe. Waziri Mkuu ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na wasimamizi wa mradi huo kwa kukamilisha mradi kwa wakati, ubora na kubakisha kiasi cha shilingi 221,636 baada ya kukamilisha mradi huo.
Mhe. Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto kuanzia umri wa miaka minne shule ili waweze kujifunza na kuangiza Shule zote hapa nchini kutenga vyumba kwa ajili ya madarasa ya awali ili watoto wadogo wasikae chini ya miti wakati wa kujifunza.
Kwa upande wake, akitoa taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Gatrida Malegesi ameeleza kuwa Shule ya Msingi Sabasita imejengwa kwa gharama ya shilingi 348, 000,000 na ujenzi wake umekamilika, imesajiliwa na imeanza kuchukua wanafunzi kuanzia Januari, 2024 na kwa wasasa wanafunzi 345.
Mwalimu Malegesi ameeleza kuwa kati ya wanafunzi waliopo, wasichana ni 169 na wavulana wapo 176 ambao baadhi yao wamepunguzwa kutoka Shule ya Msingi ambayo ilikuwepo katika kijiji hicho na shule hiyo imejengwa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Mwalimu Malegesi ameeleza kuwa shule hiyo ni sehemu ya shule zilizojengwa kwa ufadhili wa mradi wa BOOST katika Mkoa wa Mara.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mkuu leo amewasalimia wananchi wa Kijiji cha Mariwanda, ametembelea na kukagua Shule ya Msingi SabaSita, ameweka jiwe la msingi katika Mradi wa ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mkoa wa Mara, amefanya kikao cha ndani na watumishi na kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Miembeni.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa