Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo ameongoza kikao cha utambulisho wa Mpango wa M-Mama katika Mkoa wa Mara kilichofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Mzee amewataka viongozi na watendaji wa Mkoa wa Mara kutimiza wajibu wao katika maandalizi na utekelezaji wa Mpango huu ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya Mama na Mtoto.
“Kinachohitajika hapa ni viongozi na watendaji wote kutimiza wajibu wetu ili kufanikisha maandalizi na hatimaye utekelezaji wa mpango huu katika Mkoa wa wetu ili kuokoa wanawake wajawazito na watoto wachanga” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa M-Mama katika bajeti zao za mwaka wa fedha 2023/2024 pamoja na kufanya maandalizi mengine yanayohitajika ili mpango uweze kuanza mwezi Mei, 2023 katika Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa Mpango wa M-Mama utawezesha upatikanaji wa usafiri wa kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa watoto changa na wanawake wajawazito katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Mara Bibi Leah Daniel ameeleza kuwa kwa sasa upatikanaji wa huduma za afya ya mama na mtoto katika Mkoa wa Mara umeimarika na Mkoa umefanikiwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga wanaofariki.
“Kwa sasa Mkoa una vituo vya kutolea huduma za afya 335 kutoka vituo 290 mwaka 2017 na vituo hivi vyote vinatoa huduma za mama na mtoto” amesema Bibi Leah.
Bibi Leah ameongeza kuwa kati ya vituo vyote vilivyopo, vituo 35 vinauwezo wa kufanya upasuaji na kuongeza damu kwa wagonjwa huku magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) zikiwa 13 tu kwa Mkoa mzima.
Kwa mujibu wa Bibi Leah, kuanza kwa Mpango wa M-Mama utasaidia kuokoa maisha ya wanawake wajawazito na watoto wachanga baada ya kuanza utekelezaji wake kwani wananchi watapata uhakika wa usafiri wa kwenda katika vituo vya kutolea huduma kwa kundi hilo maalum.
Bibi Leah ameeleza kuwa takwimu za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa wajawazito 93,539 walijifungua katika vituo vya kutolea huduma, 344 walijifungua majumbani bila usaidizi wowote na wajawazito 131 walijifungua katika jamii kwa usaidizi wa wakunga wa jadi.
“Wengi wa wajawazito walioshindwa kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya ni kwa sababu ya kukosekana au kushindwa kumudu gharama za usafiri na hivyo kulazimika kuhatarisha maisha ya akina mama hawa” amesema Bibi Leah.
Usafiri utakaotumika kuwapeleka wajawazito na watoto vituoni ni magari, boti na meli za Serikali na watu binafsi kulingana na uhitaji wa eneo husika vitakavyokuwa vimesajiriwa na Halmashauri husika kwa ajili ya kutoa huduma hizo katika ngazi ya jamii.
Mpango wa M-Mama ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 09 Desemba, 2023 mkoani Dodoma na kuagiza kusambazwa kwa mpango huo katika mikoa yote hapa nchini.
Awali kabla ya uzinduzi rasmi, Mpango huu umefanyiwa majaribio katika Mkoa wa Shinyanga na baadhi ya Wilaya za Mkoa wa Mwanza na Serikali imejiridhisha kuhusu manufaa ya mpango huu katika kuimarisha afya ya mama na mtoto.
Kikao cha utambulisho wa M-Mama kimehudhuriwa na Dkt. Yahya Hussein kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bibi Rahma Bajir, Mkuu wa Kitengo cha M-Mama, Vodafone Foundation na watumishi wengine.
Aidha, utambulisho huo umehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Wakuu wa Idara na Vitengo vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meya na Wenyeviti wa Halmashaur za Mkoa wa Mara, Makaimu Wakurugenzi wa Halmashauri na Waganga Wakuu wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa