Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Mara kuhakikisha watoto wote chini ya miaka mitano wanapata chanjo ya ugonjwa wa polio ya matone.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Polio katika Mkoa wa Mara iliyofanyika katika Kituo cha Afya cha Nyasho, Manispaa ya Musoma, Mheshimiwa Mzee ameeleza kuwa ni vizuri watoto wote wapate chanjo ya ugonjwa wa polio.
“Mtoto asiyepata chanjo ya polio ni hatari kwake yeye mwenyewe na jamii yote inayomzunguka maana wataalamu wanasema ugonjwa huu unaambikiza na mtu akishaupata hautibiki tena” alisema Mheshimiwa Mzee.
Aidha, amewaagiza wasimamizi wa Sekta ya Afya kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanyika vizuri na kwa uaminifu ili Taifa liweze kuwa salama kutokana na uwezekano wa watu kupata ugonjwa wa polio.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mzee ameipongeza Idara ya Afya ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na wasimamizi wote wa Afya katika ngazi mbalimbali kwa kusimamia vizuri kampeni ya chanjo kwa awamu ya pili na kuuwezesha Mkoa kuvuka lengo la kuchanja kwa asilimia 119.
“Ninawapongeza sana wasimamizi wote wa sekta ya afya na wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kazi nzuri iliyofanyika katika awamu ya pili ya chanjo ya polio hapa nchini ambapo Mkoa wetu ulifanya vizuri” alisema Mheshimiwa Mzee.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Musoma Mheshimiwa William Gumbo ameeleza kuwa Manispaa ya Musoma imejipanga vizuri katika kufanikisha kampeni ya chanjo ya polio kwa muda uliopangwa.
“Katika awamu ya pili tulitarajia kutoa chanjo kwa Watoto 37,000 lakini tukavuka lengo na kuchanja Watoto 43,000 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 130 ya lengo la awali” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Mheshimiwa Gumbo ameeleza kuwa katika kampeni ya chanjo awamu ya pili, Manispaa hiyo iliwatumia Wenyeviti wa Mitaa ambao tayari Manispaa imeshafanya nao kikao kwa ajili ya kuhamasisha ushiriki wao katika Kampeni ya Chanjo awamu ya tatu.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Afya Dkt. Juma Mfanga ameeleza kuwa hii ni awamu ya tatu ya Kampeni ya Chanjo ya Polio hapa nchini baada ya mgonjwa wa polio kupatikana katika nchi ya Malawi Februari, 2022.
Dkt. Mfanga ameeleza kuwa baada ya hapo awamu ya kwanza ilikuwa ni katika mikoa inayoizunguka Malawi ambayo ni Mbeya, Njombe, Iringa, Songwe na Ruvuma ambayo ilipata chanjo mwezi Machi, 2022 na awamu ya pili ilifanyika nchi nzima kuanzia Mei 18-22, 2022.
Dkt. Mfanga ameeleza kuwa katika awamu hii ya tatu, kampeni ya chanjo itafanyika nyumba kwa nyumba kama ilivyokuwa katika awamu ya pili na katika kampeni hii hamna namna wataalamu wa afya wanaweza kutoa taarifa za uongo kuhusu chanjo kutokana na mfumo wa ufuatiliaji unaotumika.
Akizungumzia faida za chanjo hiyo, Dkt. Mfanga ameeleza kuwa chanjo hiyo inauwezo wa kukinga ugonjwa wa polio ambao hushambulia mishipa ya fahamu na kumfanya muathirika kupooza na kupata ulemavu wa kudumu.
Kampeni ya chanjo ya polio imeanza leo tarehe 1 Septemba, 2022 hadi tarehe 4 Septemba, 2022 hapa nchini kwa wataalamu wa afya kupita nyumba hadi nyumba kuchanja watoto wenye chini ya miaka mitano.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa