Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohamed Mtanda leo amefanya kikao na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mara na kuwataka wafanyakazi hao kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mtanda amewataka Wakuu wa Sehemu na Vitengo kufanya vikao na watumishi wanaowaongoza katika maeneo yao na kutenda haki katika maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa watumishi.
Mhe. Mtanda amewataka watumishi kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa pamoja katika Sehemu, Vitengo na hata Sekretarieti nzima ya Mkoa wa Mara katika utekelezaji wa majukumu.
Amewataka wafanyakazi kujenga mahusiano na mawasiliano baina yao na baina yao na viongozi wa Serikali na wanasiasa ili kuweza kufanikiwa katika utekelezaj wa majukumu yao.
Ameitaka Menejimeti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara kuandaa matukio ya kuwakutanisha watumishi nje ya ofisi ikiwa ni pamoja na ziara za watumishi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo mengine.
Mhe. Mtanda amewataka watumishi kuwa mabalozi wazuri wa namna Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hususan Serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Msalika Robert Makungu amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuzungumza na wafanyakazi na kuahidi kutekeleza maagizo yake yote aliyoyatoa.
Bwana Makungu amemshukuru kwa kuwakumbusha wafanyakazi kuongeza uwajibikaji na weledi katika utendaji wao.
Katika hatua nyingine, leo Mkuu wa Mkoa pia amefanya kikao na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Tarafa wote wa Mkoa wa Mara katika ukumbi wa uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameongoza kikao cha Tathmini ya utendaji kazi Mkoa wa Mara kilichohudhuriwa na viongozi wa Wilaya ya Menejimenti ya Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa