Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee leo amepokea vyumba vya madarasa 58, viti na meza kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.16 kwa ajili ya madarasa ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023.
Akizungumza baada ya kupokea madarasa hayo, Mheshimiwa Mzee ameipongeza Wilaya ya Serengeti kwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ubora na kwa wakati.
“Ninawapongeza wote waliohusika katika usimamizi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa haya, kazi iliyofanyika ni nzuri na nimeridhika na ujenzi huu” alisema Mheshimiwa Mzee.
Mheshimiwa Mzee pia amezipongeza shule ambazo zimepanda miti kuzunguka maeneo yao na kuzitaka shule hizo kuongeza miti zaidi ili kila mwanafunzi aweze kupata mti wake wa kuuhudumia akiwa shuleni hapo.
Hata hivyo, Mheshimiwa Mzee ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kusimamia na kuhakikisha mapungufu madogo madogo yaliyobainika yanaondolewa ili wanafunzi wanapoanza masomo mapungufu hayo yawe yameondolewa.
Mapungufu hayo ni pamoja na ubora wa viti na meza zilizotengenezwa, uingizaji wa umeme katika vyumba vya madarasa, uwekaji wa ngazi katika madarasa hayo na kufanya landscaping katika maeneo ya shule hizo.
Aidha, Mheshimiwa Mzee ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuongeza vyumba vya madarasa katika shule za sekondari za Mugumu na Rigicha ambazo zilieleza kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kutokana na uwingi wa wanafunzi katika shule hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Dkt. Vincent Mashinji ameeleza kuwa kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa kutawasaidia wanafunzi zaidi ya 7,000 wanaoanza kidato cha kwanza mwaka huu.
“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Serengeti, ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za kujenga vyumba 58 vya madarasa katika Wilaya ya Serengeti vimesaidia sana katika maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza” alisema Dkt. Mashinji.
Mheshimiwa Dkt. Mashinji amewataka wazazi wa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kuhakikisha kuwa wanapeleka watoto wao shule kwa hiari yao, wakishindwa kufanya hivyo, Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha, amewaagiza watendaji wa Vijiji, Mitaa na Kata kuhakikisha wazazi wote wenye watoto wanaotakiwa kwenda shule wanapelekwa shule ili watoto waweze kupata haki yao ya kusoma na kujifunza kulingana na umri wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Mrobanda Japan Mkoma ameeleza kuwa CCM imefurahishwa na kazi nzuri iliyofanyika ya ujenzi wa madarasa hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Mheshimiwa Mrobanda amewataka watendaji wote kuendelea kutekeleza Ilani kwa nguvu ili wananchi waweze kukuelewa na kukipenda Chama cha Mapinduzi na viongozi wake.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa na kutoa nafasi kwa wanafunzi wengi kuweza kusoma.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amekagua Shule ya Sekondari ya Rigicha (vyumba 4), Shule ya Sekondari ya Natta (chumba kimoja), Shule ya Sekondari ya Makundusi (vyumba 3), Shule ya Sekondari Mugumu (vyumba 8) na Shule ya Sekondari ya Mapinduzi (vyumba 10).
Katika ziara hiyo pia, Mkuu wa Mkoa amepata nafasi ya kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Natta na kusikiliza maoni, kero, changamoto zinazowakabili na kuzitolea ufafanuzi na mrejesho.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu, watumishi wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, viongozi wa CCM Wilaya ya Serengeti, Madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa