Mkoa wa Mara umeanza kutekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kuongeza uzalishaji wa zao la Kahawa kutoka tani 1,500 mwaka 2019 hadi tani 15,000 ndani ya miaka minne ijayo.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Malima wakati wa hafla ya kupokea miche ya kahawa 40,000 iliyotolewa na Bodi ya Kahawa nchini (TCB) kwa ajili ya kupandwa katika mashamba mbalimbali kati ya miche 100,000 ambayo bodi hiyo iliahidi kuitoa katika Mkoa wa Mara.
“Sisi tunataka tuwe mfano katika kilimo bora cha kahawa hapa nchini, tumeanza na tunazidi kuendelea. Mpango wetu ni kupanda miche angalau milioni mbili kila mwaka katika Mkoa mzima” alisema Malima.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Mara unalima kiasi kidogo cha kahawa aina ya Arabika katika wilaya za Tarime, Rorya na Butiama lakini imekuwa na ubora mkubwa na kufanikiwa kuongoza kwa ubora Afrika.
“Kama wakulima wetu watapata usimamizi mzuri wa mashamba yao, miche hii ya kahawa itawakomboa kwa kuwa inatoa mavuno mara kumi zaidi ya ile ya zamani ”alisema Mheshimiwa Malima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa hapa nchini Prof. Jamal Katundu ameeleza kuwa Tanzania inampango wa kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kutoka tani 50,000 kwa hivi sasa hadi tani 200,000 ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Katika kutekeleza adhma hii, mwaka huu tunampango kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya kupanda mashamba mawili makubwa ya mfano katika kila wilaya inayolima kahawa ambayo yatatumika kama mashamba darasa kwa wananchi wanaoyazunguka mashamba hayo”.
Ameushukuru Mkoa wa Mara kwa utayari wao katika kuongeza uzalishaji katika zao la kahawa ameahidi kuleta miche zaidi kama mikoa mingine iliyotengewa miche haitaonyesha utayari wa kuipanda miche hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde amesema kuwa kwa sasa serikali inatilia zaidi mkazo kwa vijana kujiajiri na kilimo ni fursa kubwa sana ya vijana kuweza kujiajiri kiurahisi.
Ameupongeza Mkoa wa Mara na Bodi ya Kahawa kwa jitihada za kuongeza uzalishaji wa zao la Kahawa hapa nchini. Aidha ametoa rai kwa mikoa yote hapa nchini kutenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana watakaohitaji kulima katika vikundi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa