Mkoa wa Mara umedhamiria kuboresha elimu ya Msingi na Sekondari mkoani humu kwa vitendo kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na ufundishaji na kuvunja kabisa mtandao wa wizi wa mtihani uliokuwepo miaka ya nyuma.
Akizungumza kwenye Kongamano la Wadau wa Elimu wa Mkoa wa Mara lililofanyika tarehe 23 Februari 2020, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Malima amesema tumejitahidi sana kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Akizungumzia kuhusu mtandao wa wizi wa mitihani mkoani Mara, Mheshimiwa Malima alisema “Mkoa wa Mara ulikuwa ni kitovu cha wizi wa mitihani hapa nchini, lakini tumefanikiwa kuuvunja mtandao wa wizi wa mitihani na sasa tunachokipata ndio hali halisi”. Amesema japokuwa awali Mkoa ulionyesha unafaulisha sana, lakini baadaye waligundua ufaulu huo ulitokana na wizi wa mtihani.
Mheshimiwa Malima amesema, wizi huu wa mitihani ungeachwa uendelee ungejenga kizazi cha watu wengi sana ambao hawajui chochote lakini wanavyeti vizuri. “Ingekuwa ni hatari kwa maendeleo ya taifa letu kwa siku za baadaye”. Amesema katika mtandao huo kulikuwa na uhusika wa wadau karibu wote wa elimu na hususan wazazi ambao walikuwa wanatoa fedha za kununua mitihani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mdahalo huo na Mbunge wa Musoma Vijijini Prof. Sospeter Muhongo alisema zamani Mkoa wa Mara ulikuwa na shule mbili tu za sekondari za umma Mara Sekondari na Musoma Alliance lakini zilikuwa zinafanya vizuri sana na wengi waliohitimu hapo walifaulu na kufanya vizuri sehemu nyingine walizoenda kusoma.
“Enzi zetu sekondari za binafsi zilizokuwepo chache lakini zilikuwa hazitushindi kabisa tuliokuwa tunasoma shule za serikali katika mashindano ya kitaaluma, zilitushinda katika mambo mengine”. Alisema Mhe. Muhongo. Alisema sababu kubwa zilizochangia wao kufanya vizuri ilikuwa ni ubora wa walimu waliokuwa wanawafundisha na mazingira mazuri ya kusomea katika maeneo ya shule yaliyokuwepo wakati huo.
Kongamano hilo lililofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe, lilihudhuriwa pia na wazazi, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, walimu, maafisa elimu wa ngazi za kata, halmashauri na ngazi ya mkoa. Aidha walihudhuria vyama mbalimbali ikiwemo Chama cha Walimu, Vyama vya Wakuu wa Shule, Vyama vya walimu wakuu, wanasiasa, watu maarufu na wananchi wakawaida.
Kongamano lilifanikiwa kutoa maazimio tisa ambayo ni pamoja na halmshauri ziandae mikakati ya kuboresha miundombinu ya elimu shuleni; mwanafunzi ambaye hataonekana shuleni kwa siku saba mfulilizo atalazimika kufika shuleni na mzazi wake na utaratibu wa utoaji chakula kwa wanafunzi shuleni ni lazima hivyo wazazi ambao hawatachangia chakula watachukuliwa hatua za kisheria.
Pia kongamano lilikubaliana kuwa walimu watoro wafikishwe kwenye mamlaka ya nidhamu na maamuzi yatolewe haraka ili kuimarisha uwajibikaji wa walimu; mahusiano kati ya walimu na jamii yaimarishwe ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji; vitendo vya mimba kwa wanafunzi na ukatili kwa watoto wa kike vitengenezewe mkakati wa kuvitokomeza na uwepo wa mpango bora wa kuishirikisha jamii kwenye maendeleo ya shule.
Aidha kongamali liliazimia kuwa serikali za vijiji ziwe na mkakati wa kuhakikisha usalama wa walimu kwenye mazingira yao na kongamano lingine la kutathmini maazimio ya kongamano hili lifanyike tarehe 30 Agosti, 2020.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa