Mkoa wa Mara unakabiliwa na changamoto ya upungufu mkubwa wa Maafisa Lishe jambo linalosababisha utekelezaji wa majukumu ya kusimamia hali ya lishe katika ngazi ya mkoa.
Hayo yameelezwa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tiguga wakati alipokuwa akifungua kikao cha Kamati ya Lishe ya Mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara.
“Kwa sasa Mkoa una Maafisa Lishe walioajiriwa watatu tu kati ya maafisa kumi ambao wanahitajika katika mkoa mzima”. Alisema Dkt. Tinuga.
Dkt. Tinuga ameeleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo Wakurugenzi wa Halmashauri wameteua maafisa wa kada nyingine kukaimu nafasi hizo jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kuratibu shughuli za lishe katika Mkoa wa Mara.
“Kwa sasa tunaandaa mafunzo ya siku mbili kwa maafisa lishe wote wa Mkoa wa Mara ili kuweza kuwajengea uwezo na kuwasistiza shughuli wanazotakiwa kufanya katika kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele katika bajeti, matumizi na mipango kazi ya halmashauri zote.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Mkoa wa Mara Bwana Paul Makali ameeleza kuwa kwa sasa Mkoa unakabiliwa na udumavu kwa watoto wenye chini ya miaka mitano.
“Watoto 133,507 kati ya watoto 460,368 wamedumaa, hii ni sawa na asilimia 29 ya watoto wote wenye chini ya miaka mitano katika Mkoa wa Mara wamedumaa” alisema Bwana Makali.
Aidha Bwana Makali ameeleza kuwa athari kubwa inayowapata watoto waliodumaa ni pamoja na kutokufundishika kiurahisi na hata wakiwa watu wazima hawawi na uelewa mzuri katika mambo mbalimbali.
“Tafsiri yake ni kwamba kwenye darasa la watoto 45 kuna watoto 13 ambao hawafundishiki kabisa kutokana na kukosa lishe bora hususan kwa siku 1000 za mwanzo” alisema Bwana Makali
Kikao hicho ambacho kinakaa mara nne kwa mwaka kimeazimia kuimarisha uzimamizi wa afua za lishe pamoja ikiwa ni pamoja na baadhi ya wajumbe wa kikao cha mkoa kuhudhuria vikao vya lishe vya halmashauri mbalimbali.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa