Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhehsimiwa Ally Salum Hapi leo amepokea Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Shule ya Msingi Robanda ukitokea Mkoa wa Arusha na kuanza kukimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Akizungumza mara baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru, Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara na utapitia miradi 51 kwa ajili ya kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua yenye thamani ya shilingi 18, 661, 495,564.55.
“Kati ya fedha zote za miradi ya maendeleo, shilingi milioni 515,053,140 ni mchango wa wananchi; shilingi 16,153,805,615.81 kutoka Serikali Kuu wakati shilingi 429,116,808.74 ni mchango wa Halmashauri” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa miradi ya maendeleo itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru ipo katika sekta za elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, ustawi wa jamii na viwanda na biashara.
Aidha Mheshimiwa Hapi amewakaribisha wakimbiza Mwenge kitaifa kutembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika eneo la Mwitongo.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa Mwitongo utawasha Mwenge wa Mwitongo; kutembelea kaburi la Baba wa Taifa, Makumbusho ya Baba wa Taifa pamoja na kuwasalimia wanafamilia.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa umejiandaa vizuri katika kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri zote tisa hadi tarehe 06 Julai, 2022 ambapo Mara utaukabidhi kwa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Hapi alichukua fursa hiyo kuwahamasisha wananchi waliojitokeza kwenye mapokezi ya Mwenge kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Amezitaja faida ya Sensa hiyo kuwa ni pamoja na kusaidia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa; kusaidia Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo; kuisaidia Serikali kusimamia mazingira; na takwimu zitasaidia katika ugawaji wa maeneo ya utawala” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza mpaka sasa Mkoa umetenga maeneo 3,660 ya kuhesabia watu pamoja na kuandaa nyaraka zote muhimu za sensa ambayo inatarajiwa kufanyika hapa nchini tarehe 23 Agosti, 2022.
Wakati huo huo Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambapo Mwenge umeweka mawe ya msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Morotonga; Kituo cha Afya Kenyana na kufungua Kiwanda cha kutengeneza Mafuta ya Alizeti cha Lumuye Leopard Hardware Co.
Hata hivyo, Mwenge wa Uhuru umekataa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Kijiji cha Rubanda na kuzindua madarasa katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mapinduzi kutokana na dosari mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi huo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaendelea tena kesho tarehe 28 Juni, 2022 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo; Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Maendeleo ya Kitaifa”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa