Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) leo ameendelea na ziara yake katika Wilaya za Rorya na Butiama ambapo ametembelea mradi wa maji Komuge na kuahidi kutoa shilingi milioni 720 kwa ajili ya kuboresha mradi wa maji Komuge.
Serikali imetoa ahadi hiyo baada ya kusikiliza maombi ya wananchi, Mbunge wa Jimbo la Rorya Mhe Jaffari Chege na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara Mhe. Agness Marwa ambao wameomba mradi huo uboreshwe ili wananchi waweze kupata huduma.
Akizungumza na wananchi wa eneo la Komuge Mhe. Majaliwa amesistiza adhma ya Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumtua mama ndoo kichwani na kuleta mahitaji mengine ya msingi kwa Watanzania.
Mhe. Majaliwa ameitaka RUWASA kukamilisha maboresho ya mradi huo kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji ya uhakika.
Wakati huo huo, Mhe. Waziri Mkuu ametoa wiki moja kwa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kukamilisha uchunguzi wa mwalimu wa Shule ya Msingi Kinesi B ambaye anatuhumiwa kuiba vifaa na fedha za ujenzi wa shule.
“Shule hiyo ilipewa shilingi milioni 540 hapa haijakamilika kwa sababu vifaa na fedha taslimu shilingi milioni 24 vimeibiwa na mwalimu huyo
Mhe. Waziri Mkuu amevitaja vifaa vilivyoibiwa kuwa ni pamoja na mlango wa chuma, saruji mifuko 100, mabati 80, feni 50, gypsum board 20, ndoo za rangi zenye thamani ya milioni 11, kokoto na nyaya za umeme.
Mhe. Waziri Mkuu amesema Mwalimu huyo amesababisha madeni ya shilingi milioni 9 kwa fundi wa ujenzi Victor Joseph John jambo ambalo amesema halikubaliki kwa watumishi wa umma kuchukua kiholela fedha na mali walizokabidhiwa kuzitunza.
“Watumishi wasio waadilifu wanawachafua wenzao, wanarudisha nyuma jitihada za Serikali na kukwamisha maendeleo ya wananchi, hawapaswi kuvumiliwa hata kidogo, hii ni hujuma” amesema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya Bwana Abdul Mtaka ameeleza kuwa walimtaka mwalimu atoe maelezo kwa maandishi kwa nini ameshindwa kusimamia huo mradi na kusababisha hasara, Mwalimu alileta majibu yake na kwa sasa wanaendelea na kumchukulia hatua za kinidhamu.
“Tulibaini wizi huo baada ya kupata taarifa ya Mkaguzi wa Ndani na suala hilo, kwa sasa tunasubiria matokeo ya uchunguzi wa TAKUKURU ulioanza Novemba, 2023” amesema Bwana Mtaka.
Katika Wilaya ya Rorya, Mhe. Waziri Mkuu ametembelea Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi eneo la Utegi na kuelekea Wilaya ya Tarime ambapo amefanya mkutano wa hadhara katika eneo la Sirari, kuweka jiwe la msingi katika mradi wa soko la kimkakati la Halmashauri ya Mji wa Tarime kabla ya kuhitimisha ziara yake kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Tarime.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Deo Ndenjembi na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa