Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ameahidi kutoa shilingi milioni 700 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Manyamanyama ili kukiwezesha kituo hicho kupata usajili na kuwa Hospitali ya Mji wa Bunda.
Akizungumza leo tarehe 22 Aprili 2020 baada ya kukagua Kituo cha Afya Manyamanyama na kuangalia utayari wa Halmashauri ya Mji wa Bunda kupambana na janga la Corona, Eng. Nyamanga alisema Serikali itatoa fedha hiyo ili Kituo Cha Afya Manyamanyama kiweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa wananchi wa Bunda.
“Fedha hizi zitaweza kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyobakia na kukarabati majengo ya zamani pamoja na kujenga njia ili iweze kusajiliwa kama hospitali ya Halmashauri ya Mji Bunda ili iweze kuongeza huduma zinazotolewa kwa wananchi” alisema Eng. Nyamhanga
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mji wa Bunda Bibi Janeth Peter Mayanja akiwasilisha taarifa ya Halmashauri kwa Katibu Mkuu TAMISEMI alieleza kuwa Kituo cha Afya Manyamanyama kinahudumia wananchi wengi wa Wilaya za Bunda, Wilaya ya Butiama na Musoma Vijijini hususan wanaoishi jirani na Wilaya ya Bunda.
“Pamoja na kutoa huduma kwa wananchi wengi kituo hiki kinakabiliwa na changamoto za uhaba wa miundombinu ikiwemo majengo ya mionzi, jengo la wagonjwa wa nje, mochwari na njia za kuunganisha kituo (walk ways)”alisema Bibi Mayanja.
Kituo cha Afya Manyamanyama kilijengwa na serikali miaka ya 1980 hata hivyo kutokana na upungufu wa miundombinu na huduma kilisajiriwa kama Kituo cha Afya badala ya Hospitali ya Halmashauri ambayo ilitarajiwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa