Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ameahidi kutoa shilingi milioni 100 kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe ya kuelekea katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.
Akizungumza leo tarehe 21 Aprili 2020 baada ya kupokea taarifa na kukagua hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Eng. Nyamhanga ameeleza kuwa kwa sasa ofisi yake itatoa fedha hizo ili kuwawezesha wagonjwa, watumishi na wananchi kupita sehemu nzuri wakati serikali inatafuta fedha za kujenga kwa kiwango cha lami.
“TAMISEMI itatoa milioni 100 ili kujenga barabara hii mapema iwezekanavyo ili kuifanya barabara hii ipitike kiurahisi” alisema Nyamhanga.
Aidha Eng. Nyamhanga amepongeza ubunifu uliofanywa na Wilaya ya Serengeti wa kuweka wodi za muda katika jengo la wagonjwa wa nje. “Huu ni ubunifu mzuri sana kwani unahakikisha wananchi wanapata huduma wakati hospitali ikiendelea kukamilishwa”.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Emiliana Donald ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali hiyo umekamilika na kwa sasa hospitali imeanza kutumika kutoa huduma za afya kwa wananchi.
“Majengo ya awamu ya kwanza yaliyokamilika na yanayotoa huduma ni pamoja na majengo ya mama na mtoto, utawala, kusubiria wagonjwa, lango la kuingilia hospitali, jengo la wagonjwa wa nje pamoja na barabara ya kuunganisha majengo ya hospitali” alisema Dkt. Donald.
Aidha kwa sasa hospitali hiyo inajumla ya watumishi 56 tu ambao ni nusu ya watumishi wanaohitajika kukidhi mahitaji ya Hospitali za Wilaya.
Aidha alizitaja changamoto zinazoikabili hospitali hiyo kwa sasa ni pamoja na maji, ukosefu wa wodi za kulaza wagonjwa, nyumba za watumishi, jengo la mionzi, mochwari na kichomea taka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Nurdin Babu ameeleza kuwa hospitali hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa barabara ya kuingia hospitali hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 3.
“Kwa sasa ili kuja kwenye hospitali hii, baada ya kumaliza lami tunalazimika kupita kwenye mashamba ya wananchi ili kukwepa madimbwi yaliyopo kwenye barabara hii” alisema Mheshimiwa Babu.
Mheshimiwa Babu alisema changamoto nyingine za hospitali hiyo ni pamojana gari ya kubebea wagonjwa, uzio wa kuzunguka hospitali hiyo na upungufu wa miundombinu hususan wodi za wagonjwa.
Mheshimiwa Babu alisema awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti ulianza mwaka 1974 kwa michango ya wananchi na wadau mbalimbali, lakini ujenzi huo ulimaliziwa na fedha za serikali ya Awamu ya Tano na hivi sasa umekamilika na wameanza kutoa huduma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa