Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 9 Agosti 2021 ameanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Hapi ameanza ziara kwa kutembelea Shule ya Sekondari ya Machochwe iliyopo katika Wilaya ya Serengeti na kuwaagiza Watendaji wa Vijiji na Kata kutoa taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi.
“Wananchi hawa wanatakiwa kupata taarifa sahihi za mapato na matumizi kila wakati katika vikao halali na katika mbao za matangazo” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha Mheshimiwa Hapi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kukamilisha mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Machochwe kabla ya Desemba, 2021 kuisha.
“Mmeletewa fedha za ujenzi wa kituo cha afya miezi miwili fedha imekaa tu hamjaanza ujenzi na hapa wananchi wanahangaika kutafuta matibabu” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Serengeti na kukagua wodi za wagonjwa, nyumba za watumishi na mgahawa vinavyoendelea kujengwa katika hospitali hiyo.
Aidha ametembelea mradi wa stendi ya mabasi ya Mji wa Mgumu na kuagiza Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Serengeti kuchunguza mradi wa ujenzi wa stendi hiyo.
“Haiwezekani choo cha matundu 10 na mabafu mawili kinajengwa kwa shilingi milioni 45 ambayo ni sawa na wastani wa shilingi milioni 3,300,000 kwa kila tundu la choo, hii haikubaliki” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa hajaridhishwa na mradi huo kwani ni fedha nyingi zimetumika lakini majengo ni ya kawaida tu ila gharama zilizotumika ni kubwa.
Mheshimiwa Hapi ametembelea eneo la mradi wa Uwanja wa Ndege wa Mugumu na kumwagiza Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji kukamilisha mchakato wa ndani na kukamilisha ndani ya mwezi mmoja ili mazungumzo ngazi nyingine yaweze kuanza.
Mkuu wa Mkoa pia ametembelea Shule ya Msingi Mapinduzi B na kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na kuahidi kupeleka mifuko 20 ya sementi kwa ajili ya kukamilisha darasa moja lililojengwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amehitimisha ziara yake kwa kuzungumza na wananchi wa Mji wa Mgumu katika uwanja wa Right to Play ambapo alitumia muda mwingi kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Hapi ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Serengeti, Mbunge wa Serengeti, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, watumishi na viongozi wa wilaya, tarafa na kata.
Kesho ziara ya Mkuu wa Mkoa inategemea kuendelea katika Wilaya ya Serengeti ambapo atatembelea kata za Natta, Manchira, Ikoma na Stendi Kuu kukagua miradi ya maendeleo na kuweka mawe ya msingi katika baadhi ya miradi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa