Mwakilishi wa Mkuuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Maulid Sulumbu leo amefunga rasmi mashindano ya Nyama Choma Festival Wilaya ya Tarime yaliyofanyika katika mnada wa Mtana, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kuwataka wafugaji wa Mkoa wa Mara kufanya ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija katika ufugaji wao.
Mhe. Sulumbu amesema hayo alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi katika ufungaji wa mashindano ya Nyama Choma Festival na kuwahimiza wafugaji kuchangamkia fursa inayoletwa na mashindano hayo katika Mkoa wa Mara.
“Lengo la kuanzisha mashindano haya ni kutangaza fursa zinazopatikana katika Mkoa wa Mara na hususan uwepo wa mifugo mingi ambayo ina nyama bora kutokana na aina ya mbegu ya mifugo na ufugaji unaofanyika katika Mkoa wa Mara” amesema Mhe. Sulumbu.
Mhe. Sulumbu amewahimiza wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya kusindika nyama, ngozi na mazao mengine ya mifugo katika Mkoa wa Mara ili kutoa soko la uhakika kwa wafugaji na wachuuzi wa mifugo wa Mkoa wa Mara.
Kanali Sulumbu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, amechukua fursa hiyo kuwashukuru washiriki wa mashindano na wadhamini wa mashindano hayo kwa kujitokeza kwao kufanikisha Nyama Choma Festival katika Wilaya ya Tarime.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa majaji katika mashindano hayo Bwana Gambaless Timotheo amesema washiri wa mashindano hayo walikuwa sita na amemtaja mshindi wa mashindano hayo kuwa ni Charles Joseph Mniko maarufu kama Chale Nyama ambaye amejishindia shilingi 500,000.
Bwana Timotheo amemtaja mshindi wa pili kuwa ni Bwana Christopher maarufu kama Miti Mirefu ambaye ameshinda shilingi 300,000 huku Mombasa Nyamachoma akiwa mshindi wa tatu ambaye ameshinda shilingi 200,000.
Bwana Timotheo amewataja washiriki wengine walioshiriki mashindano hayo kuwa ni Rajusa Trading and food points aliyeshika nafasi ya nne; Peter Okinda nafasi ya tano wakati Emmanuel Siguda ameshika nafasi ya sita na kuwapongeza washiriki wote kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Bwana Timotheo amevitaja vigezo vya washindi kuwa ni pamoja na kusajiriwa kama mshiriki wa mashindano, usafi wa mazingira, usafiri binafsi wa wapishi, ubora wa nyama na vikolombwezo vya kwenye nyama kama vile pilipili, kachumbari na huduma kwa wateja.
Kwa upande wake, mshindi wa mashindano hayo Bwana Charles Joseph Mniko amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo amesema ni mara ya kwanza kufanyika mashindnao ya kuchoma nyama katika Wilaya ya Tarime.
Bwana Mniko amesema amekuwa katika biashara ya kuchoma nyama kwa miaka 30 sasa lakini hakuwahi kushiriki katika mashindano kama hayo na anawashukuru waandaaji kwa kuanzisha fursa nzuri kwa wafanyabiashara kupanua uzoefu wao.
Bwana Mniko amewaomba waandaaji kuendelea kuandaa mashindano mengine kama hayo katika Wilaya ya Tarime ilikutoa fursa kwa wachoma nyama wengi zaidi kujitokeza na kuleta ushindani ambao utaboresha biashara yao.
Mashindano hayo yamehudhuriwa pia na viongozi wa Halmashauri za Wilaya ya Tarime, Wakurugenzi wa Tarime TC, Tarime DC, Bunda TC, Butiama DC na Rorya DC maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri za Mji wa Tarime na Wilaya ya Tarime na Halmashauri nyingine za Mkoa wa Mara.
Hii ni mara ya pili kwa Nyama Choma Festival kufanyika katika Mkoa wa Mara baada ya kufunguliwa katika mnada wa Kiabakari, Butiama na mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika pia kesho tarehe 4 Julai, 2024 Wilaya ya Musoma katika stendi ya mabasi ya Bweri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa