Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa Mhe. David Ernest Silinde leo amehitimisha ziara yake Mkoa wa Mara kwa kuzipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kwa kazi nzuri ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Mheshimiwa Silinde ametoa pongezi hizo katika maeneo tofauti tofauti baada ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Halmashauri ya Mji wa Tarime na Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mheshimiwa Silinde ametembelea Shule ya Sekondari ya Nyabisaga (madarasa 3), Shule ya Sekondari ya Nyantira (madarasa 2), na Shule ya Sekondari ya Kemambo (darasa 1) yote yakiwa katika hatua za ukamilishaji.
Mheshimiwa Silinde akiwa katika Shule ya Sekondari ya Kemambo amemtaka Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara kutoa motisha kwa Shule ya Sekondari ya Kemambo kwa kukamilisha mapema ujenzi wa madarasa ambapo Waziri alikuta mafundi wakiendelea kufanya usafi baada ya kazi ya ujenzi kukamilika.
Katika Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mheshimiwa Silinde ametembelea Shule ya Sekondari ya Nyamisangura ambayo awali ilipewa fedha za kujenga vyumba 11 vya madarasa, lakini baadaye vyumba vitano kati ya hivyo vilihamishiwa katika Shule ya Sekondari ya Turwa B na shule hiyo kubaki na vyumba sita vya madarasa.
Hata hivyo, vyumba vitatu vilikuwa kwenye uezekaji wakati vyumba vitatu vingine vikiwa kwenye lenta jambo ambalo halikumfurahisha Mheshimiwa Naibu Waziri.
Naibu Waziri pia alitembelea Shule ya Sekondari ya Bunda (madarasa 3) na Shule ya Sekondari ya Nyamikokoto ambayo inajengwa mpya kupitia mradi wa SEQUIP katika Kata ya Bunda Stoo ambayo itachukua wanafunzi wa Kata ya Bunda Mji na Kata ya Bunda Stoo.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri aliambatana na Wakuu wa Wilaya za Tarime na Bunda, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala Wasaidizi Sehemu ya Elimu na Sehemu ya Miundombinu, Mbunge wa Tarime Vijijini, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri, watumishi wa Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa