Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Said Mohammed Mtanda leo tarehe 25 Mei, 2023 amewasili Mkoani Mara na kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee katika hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Awali, viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Mara, Kamati ya Usalama ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, wamempokea Mheshimiwa Mtanda katika eneo la Ndabaka, Wilaya ya Bunda.
Baada ya mapokezi, Mhe. Mkuu wa Mkoa amefika katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kwa ajili ya kutia saini kitabu cha wageni na kujitambulisha na kuzungumza na viongozi wa Chama cha Mapinduzi.
Msafara wa Mkuu wa Mkoa ulielekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo alipokelewa na viongozi wa taasisi za Umma, Wakuu wa Idara na Vitengo, watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na viongozi wa CCM Mkoa wa Mara.
Hafla fupi ya makabidhiano ilifanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee alimkabidhi ofisi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi, Mheshimiwa Mtanda amewataka viongozi na watumishi wote kushirikiana na kufanyakazi kwa ubunifu, uadilifu na uaminifu ili kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ufanisi.
“Sisi sote tuna wajibu wa kutekeleza ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Mara na ndio maana tupo hapa katika Mkoa huu, tutimize wajibu wetu” alisema Mheshimiwa Mtanda.
Aidha, ametumia nafasi hiyo Kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mhe. Mtanda amehitimisha siku kwa kushiriki katika Kikao cha Kamati ya Siasa ya Manispaa ya Musoma na Viongozi wa Mitaa na Kata za Manispaa ya Musoma.
Mhe. Mtanda aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 23 Mei, 2023 na kuapishwa rasmi tarehe 24 Mei, 2023.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa