Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi leo amezindua zoezi la kujiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Mara kwa kujiandikisha katika kituo kilichopo Ofisi ya Kata ya Mkendo, Manispaa ya Musoma.
Akizungumza baada ya kujiandikisha, Mhe. Mtambi amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia leo hadi tarehe 20 Oktoba, 2024 kwenye vituo vilivyopo katika maeneo yao.
“Ninawasihi wananchi kujitokeza kujiandikisha ili kutumia fursa hii ya kikatiba kuwachagua viongozi watakaowahudumia na kuwaletea maendeleo katika vijiji, mitaa na vitongoji vyenu” amesema Mhe. Mtambi.
Mhe. Mtambi amesema zoezi la uandikishaji linafanyika kwa muda mfupi sana na hivyo wananchi hawana sababu ya kutokushiriki kujiandikisha ili waweze kushiriki kuchagua na kuchaguliwa kuwa viongozi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Juma Chikoka ambaye pia amejiandikisha katika kituo hicho amewataka wananchi wa Wilaya ya Musoma kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuwawezesha kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Mhe. Chikoka amesema hii ni fursa kwao kujiandikisha ili kuweza kuchagua viongozi na kuchaguliwa kuwa viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji mbalimbali.
Baada ya kujiandikisha Mhe. Chikoka amekagua zoezi la uandikishaji katika Manispaa ya Musoma na kutembelea maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika hapa nchini 27 Novemba, 2024 na zoezi la kujiandikisha limeanza leo na mwisho ni tarehe 20 Oktoba, 2024 na sifa za mtu kujiandikisha ni awe raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa mtaa, kijiji au kitongoji ambapo uchaguzi unafanyika.
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti wa Mtaa, wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi mchanganyiko) na kundi la wananwake hii ni kwa Halmashauri za Mji na Manispaa wakati katika Halmashauri za Wilaya nafasi zinazogombewa ni Mwenyejiti wa Kijiji, wenyeviti wa vitongoji vilivyomo katika Kijiji na kundi la wanawake.
Hafla ya uzinduzi imeshuhudiwa na watumishi kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma pamoja na wananchi waliokuwepo katika eneo hilo.
Kauli mbiu ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu ni “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi”.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa