Serikali imeutaka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kulipa faini ya shilingi bilioni moja ndani ya siku 14 baada ya bomba lake la maji machafu kuachia na kutiririsha maji machafu karibu na makazi ya watu katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.
Akisoma faini hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel G. Mafwenga, amesema kuwa faini hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha 187 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.
“Faini hii isaidie kuikumbusha migodi yote hapa nchini wajibu wao wa kulinda mazingira na kuhakikisha kwamba jambo kama hili halitajirudia tena wakati mwingine” alisema Dkt. Mafwenga.
Dkt. Mafwenga ameeleza kuwa japokuwa maji machafu hayo yalikuwa hayana sumu kama ilivyotaarifiwa awali, lakini maji hayo sio salama kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya binadamu.
Akizungumza baada ya kukagua na kupata maelezo ya eneo hilo, Waziri wa Madini Mheshimiwa Dotto Biteko ameutaka mgodi huo kuimarisha mahusiano baina yake na wananchi wa eneo la Nyamongo ulipo mgodi huo.
“Malalamiko mengi yaliyopo hapa leo yanatokana na mahusiano mabovu yaliyokuwepo kati ya mgodi na wananchi wa Nyamongo. Mahusiano na wananchi yakiwa mazuri yatakuwa na faida kwa Mgodi na wananchi wanaouzunguka mgodi huu” amesema Mheshimiwa Biteko.
Mheshimiwa Biteko ameeleza kuwa suala la bomba la maji machafu kupasuka na kutiririsha maji muda mrefu bila uongozi wa mgodi kujua limetokana na uzembe na sio bahati mbaya.
“Leo akiingia mwananchi katika eneo la mgodi na kujaribu kuiba ndani ya nusu saa atakuwa ameshakamatwa, lakini bomba la maji machafu linaachia na kutiririsha maji machafu kwa masaa zaidi ya manne bila Menejimenti ya Mgodi kujua ni uzembe” alisema Mheshimiwa Biteko.
Mheshimiwa Biteko pia ameagiza kuondolewa mara moja kwa Afisa Mgodi Mkazi ambaye alikuwa ni mwakilishi wa Wizara ya Madini katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kutokana na uzembe huo.
Kuhusu malipo ya fidia ya maeneo ambapo mgodi unataka kuyachukua, Mheshimiwa Biteko ameeleza kuwa wananchi wa Nyamongo wanatumiwa na watu wachache wenye nia ovu kusitisha zoezi la tathmini na hivyo kwa sasa hawawezi kulipwa fidia mpaka tathmini ikamilike.
Mheshimiwa Biteko ameeleza kuwa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) shilingi bilioni 5 zinazotolewa na mgodi huo zitekeleze miradi ya maendeleo kwa wananchi.
“Mimi ninakuomba Mkuu wa Mkoa, hili jambo ndani ya wiki mbili liishe na miradi ya maendeleo ya wananchi ianze kutekelezwa, watu wa Nyangongo wanaulaumu mgodi kumbe mgodi ulishatoa fedha hizo” alisema Mheshimiwa Biteko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi ameeleza kuwa miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Uwajibikaji kwa Umma (CSR) kupitia Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) zilikuwa zinatumika vibaya kutekeleza miradi ndio maana Kamati hiyo ameivunja rasmi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa miradi hiyo itaanza kutekelezwa mara baada ya miradi hiyo kuwa imepitishwa na mamlaka za Serikali ambao ndio itawajibika kama utekelezaji ukiwa mbaya.
“Tunataka miradi yenu ikamilike kwa wakati, wananchi msitumike kama kichaka kwa watu kuchukua fedha za miradi ya maendeleo kwa manufaa yao binafsi” alisema Mheshimiwa Hapi.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa uongozi wa Mkoa umejipanga vizuri na ndani ya muda mfupi ujao miradi iliyokuwa imependekezwa itaanza kutekelezwa chini ya usimamizi wa Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Bomba la maji machafu yanayotoka kwenye miamba liliachia kwenye maungio yake yakiwa yanaenda kwenye bwawa la kuyasafisha tarehe 23 Aprili 2022 katika eneo la Nyamwaga na kuzua taharuki kuwa maji hayo yalikuwa yana sumu.
Hata hivyo Mamlaka za Serikali zimethibitisha kuwa maji hayo ni machafu lakini hayana sumu kama ilivyokuwa imedhaniwa hapo awali na kuzua taharuki miungoni mwa wananchi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa