Meya wa Manispaa ya Musoma Mhe. William Gumbo leo ameongoza mazoezi ya watumishi wa Serikali Mkoa wa Mara yaliyofanyika katika Uwanja wa Posta, Manispaa ya Musoma na kuwataka watumishi kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya watumishi ili kulinda afya zao.
Mhe. Gumbo amewataka watumishi kutenga siku za kufanya mazoezi katika ratiba zao na kila jumamosi ya mwisho wa mwezi, mazoezi yatafanyika kwa pamoja katika uwanaja huo.
“ Pamoja na kufuata maelekezo ya viongozi wa kitaifa, mazoezi ni muhimu kwa afya za watumishi na yanatusaidia kujenga na kulinda miili dhidi ya magonjwa na kuboresha muonekano wa mtumishi” amesema Mhe. Gumbo.
Mhe. Gumbo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kuwakumbusha wafanyakazi kufanya mazoezi na kuandaa ratiba ya mazoezi hayo na kuwataka wananchi wa Manispaa ya Musoma kushiriki katika mazoezi hayo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa mazoezi kwa watumishi ni muhimu sana kwani yanaboresha afya za watumishi na kuwalinda dhidi ya magonjwa yasiyo yakuambukizwa.
Dkt. Masatu amewashukuru viongozi kwa kuandaa mazoezi hayo kwa watumishi na kuwahimiza watumishi kushiriki kikamilifu kwa faida yao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma Bwana Ally Seif Mwendo amewapongeza watumishi wote walioshiriki kufanya mazoezi na kuwataka watumishi wa Manispaa ya Musoma kuhudhuria mazoezi hayo kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa.
Mazoezi hayo yaliwahusisha watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Manispaa ya Musoma na taasisi mbalimbali zilizopo Manispaa ya Musoma yalianza kwa mbio nyepesi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na kuuzunguka mlima Mkendo hadi Uwanja wa Posta ambapo watumishi walifanya mazoezi ya viungo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa