Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele amewaongoza maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Mara kushiriki Serengeti Utalii Nyama Choma Festival na kuwahamasisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024.
Akizungumza katika tamasha hilo lililofanyika katika eneo la mnadani, Mjini Mugumu Mhe. Gowele amewataka wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi kwa kupiga kura na kuchagua viongozi wakataowaongoza katika maeneo yao.
“Pamoja na kwamba tumejiandikisha na tumepiga kura ndani ya vyama vya siasa, tusipopiga kura siku ya uchaguzi haitakuwa na maana kwa sababu hatutaweza kuwachagua viongozi tunaowataka watakaotuletea maendeleo katika maeneo yetu” amesema Mhe. Gowele.
Mhe. Gowele amewataka wananchi kushiriki katika kampeni zitakazofanyika ili kuwafahamu wagombea wanaowania nafasi mbalimbali na kujua sera zao kabla ya kupiga kura ili kupata uelewa mpana kuhusu wagombea wanaowania nafasi mbalimbali.
Mhe. Gowele amewataka wananchi kulinda amani na utulivu na hususan wakati huu wa uchaguzi na kuwahakikisha kuwa Serikali itahakikisha kuwa kuna kuwepo amani na utulivu muda wote na watakaoanzisha uvunjifu wakati huu watachukulia hatua kali za kisheria na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi kama kuna jambo lolote wamebaini katika maeneo yao.
Aidha, Meja Gowele amewataka wananchi kutunza mazingira katika maeneo yao na kutokomeza ujangili ili kuhifadhi maliasili za Tanzania ili nchi iweze kupata manufaa ya kiuchumi yanayotarajiwa kwa kuhifanyi maliasili hizo zilizopo katika maeneo mbalimbali.
Mhe. Gowele amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi kwa mawazo yake ya kuanzisha nyama choma festival ambayo inawainua wajasiriamali wadogo wadogo na wachoma nyama waliochangamkia fursa katika Mkoa wa Mara.
Meja Gowele amewahamasisha wajasiriamali kujiunga kwenye vikundi ili waweze kufaidika na mikopo inayotolewa na Halmashauri, Serikali na wadau wengine ili kuboresha biashara zao na hali zao za maisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Kemirembe Lwota amewashukuru wananchi wa Serengeti kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye orodha ya wakazi na kuwahamasisha kushiriki kupiga kura ili kuweza kuwachagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
“Ninawasihi tujitokeze kwa wingi, tupige kura ili kupata viongozi bora watakaosimamia maendeleo katika maeneo yetu” amesema Mhe. Lwota.
Mhe. Lwota amewashukuru wadhamini waliofanikisha tamasha hilo kwa michango yao waliyoitoa ili kufanikisha tamasha hilo ambao amewataja kuwa ni Nyansaho Foundation, Grumeti Fund, TAWA, SENAPA, Wanyancha Pub na kadhalika.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Nyansaho Foundation Bibi Esther Mng’ori ambao walikuwa wadhamini wakuu wa tamasha hilo ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kwa kuwashikirisha katika maandalizi ya tamasha hilo kama wadhamini na washiriki.
Amesema taasisi yao inahusika na utoaji wa huduma na misaada kwa kushirikiana na Serikali katika elimu, afya na watu wenye mahitaji maalum katika Wilaya ya Serengeti.
Tamasha hilo lilianza na mbio na mazoezi ya viungo asubuhi na kufuatiwa na mashindano mbalimbali ya michezo na kuhitimishwa na mashindano ya uchomaji wa nyama na kupambwa na burudani zilizotolewa na wasanii mbalimbali.
Katika tamasha hilo pia, Meja Gowele alitoa zawadi kwa washindi wa mbio, michezo mbalimbali iliyokuwa inashindaniwa na mashindano ya kuchoma nyama katika tamasha hilo.
Wengine walioshiriki katika tamasha hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti, baadhi ya Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, taasisi za umma na binafsi na wafanyabiashara.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa