Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu, leo amefungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa kazi kwa Wasimamizi wa Elimu Mkoa wa Mara na kuwapongeza kwa kubuni kikao hicho cha kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Sekta ya Elimu kwa kila robo mwaka.
Akizungumza katika kikao hicho Dkt. Masatu amewataka wasimamizi hao kufanya vikao kama hivyo katika ngazi za Halmashauri na shule zilizopo ili kuboresha elimu katika Mkoa wa Mara.
“Ninaipongeza sana Sehemu ya Elimu kwa kuanzisha vikao vya tathmini ambavyo vinafanyika katika kila robo kwa ngazi ya Mkoa ni jambo zuri na la kuigwa kwa Sehemu na Vitengo vingine katika utekelezjai wa majukumu yao” amesema Dkt. Masatu.
Dkt. Masatu amepongeza kikao hicho kujadili suala la utoaji wa chakula mashuleni ambalo amesema kuwa ni muhimu sana katika utekelezaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa Chakula masuleni na mkataba wa lishe wa Kitaifa.
Dkt. Masatu ametaka kuwepo na mipango thabiti ya utekelezaji na usimamizi wa shughuli za elimu na kuzihusisha sekta nyingine pale inapohitajika.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bwana Bulenga Makwasa ameeleza kuwa Sehemu ya Elimu imeanzisha utaratibu wa kufanya vikao vya tathmini katika kila robo mwaka ili kuinua ubora wa elimu na kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zinakwamisha maendeleo ya elimu.
“Kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 tumeanza kufanya tathmini hizi ambazo zinawahusisha Maafisa Elimu wote wa Halmashauri pamoja na wasaidizi wao ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya elimu katika Mkoa wa Mara” amesema Bwana Makwasa.
Bwana Makwasa amesema katika kikao hicho mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo taarifa ya tathmini ya utekelezaji wa KPI katika robo ya pili ya mwaka 2024 ya kila Halmashauri itakayowasilishwa na Maafisa Elimu wa Halmashauri.
Bwana Makwasa amesema jambo linguine litakalojadiliwa ni taarifa ya maandalizi ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima, 2024 ambapo Maafisa Elimu wa Halmashauri watawasilisha maandalizi ya kila Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa