16 Aprili 2020
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima leo amefanya mazungumzo na viongozi wa madhehebu na jumuiya mbalimbali za kidini wanaofanya shughuli zao katika Mkoa wa Mara.
Akizungumza wakati wa kikao na viongozi hao Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa Tanzania na ulimwengu wote tupo katika mapambano makubwa dhidi ya janga la homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona maarufu kama COVID 19.
“Leo tumewaita hapa kutokana na umuhimu wenu katika masuala ya kiimani mnayoyaongoza katika jamii inayowazunguka” alisema Malima.
Alieleza kuwa pamoja na mambo mengine viongozi wa Mkoa wa Mara wanatarajia viongozi wa dini pamoja na kuliombea taifa, wasaidie katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa Corona hapa nchini na hususan kwa wananchi wanaowahudumia.
“Ninawashukuru sana viongozi wote wa dini kwa maombi yenu ya kuliombea taifa hili mnayoendelea nayo, tunaendelea kumwomba Mungu atusikie kilio chetu” alisema Mheshimiwa Malima.
Akizungumza katika mkutano huu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tinuga ameeleza kuwa viongozi wa dini wanatakiwa kuendelea kupata elimu sahihi ya corona na kuisambaza kwa waumini wao ili kuwakinga na janga la corona.
Dkt. Tinuga amewataka viongozi hao kubuni njia mbalimbali za kuwaelimisha waumini ikiwa ni pamoja na nyimbo na kuonyesha mifano ya namna ya kujikinga na corona.
“Itakuwa vizuri kama kwenye kila ibada au swala, waumini wakapata nafasi hata ya dakika 10 kuambiwa habari za janga la Corona na namna ya kujikinga.
Kwa upande wake Askofu Michael Msoganzila wa Jimbo Katoliki Musoma alieleza kuwa kutokana na janga hili kanisa hilo limebadilisha sana namna ya kuendesha misa na kupunguza baadhi ya vitu ambavyo sio vya lazima.
Aidha Kanisa limetunga sala ambayo husaliwa katika kila familia kuliombea taifa na waumini wote na kumuomba Mungu aliepushe taifa katika janga la Corona.
“Hata hivyo kuna taasisi za elimu ambazo zinamilikiwa na taasisi ya dini ambazo kutokana na athari ya majanga ya corona itakuwa ngumu kuwalipa wafanyakazi wao mishahara hususan kama janga hili litaendele kwa muda mrefu” alisema Mloganzila
Kwa upande wake Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mara Bwana Sheikh Msabaha Kassimu ameeleza kuwa anashukuru kuwa serikali imeruhusu masuala ya dini yaendelee wakati huu, na wao wanachukua tahadhari zote za kujikinga na corona.
Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, maafisa waandamizi na wataalamu mbalimbali wa afya.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa