Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma Bwana Ally. S. Mwendo leo amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara katika uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti wenye umri wa miaka 9-14 kimkoa iliyofanyika katika Shule ya Msingi Mkendo.
Akizungumza katika uzinduzi wa zoezi hilo, Bwana Mwendo amewatakaa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wakike wanapata chanjo hiyo kwani ni salama na inatolewa bure katika shule za msingi na sekondari na vituo vya kutolea huduma za afya.
“Chanjo hii inatolewa katika kampeni hii ya siku tano za wiki ya chanjo duniani, ni ile ile inayotolewa wakati wote na inatolewa bure, haina madhara na nimuhimu sana kwa mabinti ili kujikinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi hapa nchini” amesema Bwana Mwendo.
Ameitaja kauli mbiu ya zoezi hilo kuwa ni Jamii inayochanjwa, Jamii yenye afya na kuwataka wananchi kuachana na imani potofu na taarifa zisizo rasmi na badala yake wawasikilize suhauri wa wataalamu wa sekta ya afya.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii Dkt. Zabron Masatu ameeleza kuwa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameandaa chanjo ya saratani ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 9-14.
Dkt. Masatu ameeleza kuwa utoaji wa chanjo hiyo katika Mkoa wa Mara umeanza tarehe 22-26 Aprili, 2024 kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi saa 10 jioni katika shule za msingi, sekondari na katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa mujibu wa Dkt. Masatu jumla ya wasichana 229,249 wenye umri wa miaka 9-14 wanategemewa kupatiwa chanjo hiyo katika Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Uzinduzi wa zoezi la chanjo umehudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Musoma, Wasimamizi wa Afya, Maafisa Elimu na watumishi wengine ngazi ya Mkoa na Manispaa ya Musoma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa