Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo amezindua utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusu anuani za makazi.
Mheshimiwa Hapi amezindua utekelezaji huo leo katika ukumbi wa uwekezaji ambapo ametoa mwisho wa utekelezaji wa mradi huo kwa Mkoa wa Mara kuwa tarehe 1 Aprili 2022.
“Mheshimiwa Rais katika maelekezo yake amesema mwisho wa kutekeleza jambo hili kitaifa ni tarehe 1 Mei, 2022 lakini sisi kwa Mkoa wa Mara mwisho ni tarehe 1 Aprili 2022 ili kutoa nafasi ya tathmini na kuandaa taarifa ya Mkoa kabla ya tarehe 1 Mei, 2022 alisema Mheshimiwa Hapi.
Mkuu wa Mkoa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa zoezi hilo kila baada ya wiki mbili kuanzia sasa.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa zoezi la uwekaji wa anuani za makazi ni muhimu sana kwa ajili ya utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ambayo inategemewa kufanyika mwezi Agosti, 2022 hapa nchini.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, vibao vya mtaa, vijiji na makazi binafsi serikali haitavitengeneza na badala yake wananchi watatengeneza vibao hivyo wao wenyewe.
Amewataka Wakuu wa Wilaya na Halmashauri kufanya mikutano ya kuwaelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo na namna wanavyoweza kushiriki.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa katika utekelezaji wa suala hilo, Wakala wa Barabara (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wanatakiwa kuweka vibao vya mitaa inayogusana au inayochepuka kutoka barabarani katika barabara zote zinazojengwa sasa hivi au zitakazojengwa kuanzia sasa.
Mheshimiwa Hapi amezitaka Wilaya kuunda kamati maalum za utekelezaji wa zoezi hilo kuanzia ngazi za wilaya hadi katika vijiji na mitaa ili kufanikisha zoezi hilo.
Aidha amezitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa kila mtaa, Kijiji, maeneo ya biashara na makazi ya watu yanakuwa na vibao vya kuyatambulisha vinavyosomeka na kuonekana kiurahisi.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa katika kutekeleza zoezi hilo serikali italeta fedha zenye maelekezo kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo, “hazitatumika kama fedha za OC, hizi zitakuwa na maelekezo maalum” alisema Mheshimiwa Hapi.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuwa Halmashauri zitoe msaada katika zoezi hili kwani zoezi linatakiwa kufanywa na watumishi wa umma na sio watu wa nje ya serikali” alisema Mheshimiwa Hapi.
Awali, akisoma taarifa kuhusiana na miongozo ya serikali kuhusu anuani za makazi, Kaimu Afisa TEHAMA wa Mkoa Bwana Amon Stephano Mwasambungu ameeleza kuwa katika kutekeleza zoezi hilo mfumo utakaotumika unasomana na GPS.
“Kwa hivyo baada ya kazi uthamini utafanyika katika ngazi mbalimbali hivyo zoezi linatakiwa kufanywa kwa umakini, uadilifu na ukweli katika ngazi zote” alisema Bwana Mwasambungu.
Bwana Mwasambungu amezitaka Halmashauri kuwashirikisha Maafisa TEHAMA wa Halmashauri katika Kamati za kutekeleza jukumu hilo ili kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Bwana Mwasambungu amezitaka Halmashauri kutumia miongozo iliyotolewa na Serikali kuhusiana na anuani za makazi na ili kufanikisha zoezi hilo.
Zoezi la uwekaji wa anuani za makazi kitaifa lilianza mwaka 2017 katika baadhi ya mikoa hata hivyo kwa mwaka huu zoezi hilo litafanyika nchi nzima kuanzia tarehe 18 Februari 2022 hadi tarehe 01 Mei, 2022.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa