16 Aprili 2020
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima leo amezindua zoezi la kunyunyuzia dawa ya kudhibiti Corona kwenye magari ya abiria katika setendi kuu ya mabasi ya Bweri iliyopo Musoma Mjini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo Mheshimiwa Malima amewataka wamiliki wote wa magari ya abiria kuhakikisha kuwa magari yote yananyunyuziwa dawa kabla ya kuondoka stendi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa magari hayo.
“Sisi kama serikali tuhakahikisha kila mmiliki na dereva wa magari anafuata utaratibu tuliojiwekea katika Mkoa wa Mara ili kuendelea kuwakinga watu wanaotumia magari haya” alisema Malima.
Aidha aliwahimiza wananchi wote kufuatilia maelekezo yote ya wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kunawa mikono, kuchukua tahadhari mbalimbali za kujikinga.
“Suala la kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka ni muhimu sana wakati huu na japokuwa linaonekana ni jambo rahisi likifanyiwa mzaha litawaathiri watu wengi zaidi.”
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa akiwa stendi ya Bweri alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu shida ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
Akijibu malalamiko hayo, Mheshimiwa Malima amewataka Mamlaka ya Maji Musoma (MUWASA) kuhakikisha maji yanapatikana kwa urahisi katika stendi hiyo ili kuwanusuru wananchi na wasafiri wanaotumia stendi hiyo kujikinga na corona na magonjwa mengine ya mlipuko.
Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi huo aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, viongozi wa wilaya ya Musoma Mjini na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Florian Tinuga alisema zoezi hilo litafanywa katika stendi zote za Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 16 Aprili 2020.
Aidha ameeleza kuwa utaratibu unataka magari kunyunyuziwa dawa nusu saa kabla ya kuanza kupakia abiria katika magari hayo.
“Hatua hii ni muhimu kwa ajili ya kuwalinda abiria na wafanyakazi wa magari haya ambao wanakutana na watu wengi waliotoka sehemu mbalimbali ili waweze kujilinda na corona” alisema Dkt. Tinuga
Katika utaratibu huu wa kupuliza magari dawa, wamiliki wa magari watatozwa shilingi 5000 kwa mabasi makubwa, 3000 kwa basi ndogo (coaster) na shilingi 2000 kwa mabasi madogo madogo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa