Mkoa wa Mara leo umezindua rasmi Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMAM) -2021/2022-2025/2026 na kuzitakaa Halmashauri na wadau wote kuweka katika mipango na bajeti masuala muhimu katika utekelezaji wa mpango huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mhe. Dkt. Khalfan Haule amezitaka taasisi za umma, dini na mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana katika kutekeleza programu hiyo.
“Serikali inaamini kuwa msingi mzuri wa watoto unajengwa katika miaka ya awali ambayo ni 0-8 na baada ya hapo kumbadili mtoto ambaye hakupata malezi stahiki inakuwa ni vigumu sana, kwa hiyo tushirikiane kuwatunza watoto” amesema Mhe. Haule.
Aidha, Dkt. Haule amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara kuzindua Programu hiyo katika ngazi ya Halmashauri kabla ya tarehe 30 Novemba, 2023 na kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia utekelezaji wa Programu hii katika Halmashauri zao.
Dkt. Haule amesema maeneo makubwa matano ambayo yamepewa kipaumbele katika programu hii ni pamoja na lishe bora, afya bora, malezi yenye mwitikio, ulinzi na usalama wa mtoto na fursa ya ujifunzaji wa awali.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Marco Maduhu amewashukuru viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuitikia wito na kuhudhuria katika uzinduzi huo.
Aidha, Bwana Maduhu ameahidi kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa kuhusiana na programu hiyo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Mara.
Aidha, Bwana Maduhu amewaomba viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa watoto wanalelewa katika mazingira mazuri na kuhakikishiwa usalama wao.
Bwana Maduhu amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuwekeza katika malezi, makuzi na maendeleo ya watoto lakini ili kufanikisha hilo ushiriki wa wadau wa maendeleo ni muhimu sana.
Uzinduzi wa program hiyo umehudhuriwa pia na Bibi Agness Mbiu mwakilishi wa Wizara ya Afya, Bibi Mariam Luka Mwakilishi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Programu ya PJT MMAM imezinduliwa kitaifa mwaka jana ikiwa na kauli mbiu ya Mtoto Kwanza inategemea kuunganisha jitihada zilizokuwa zinafanywa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kuanzia miaka 0-8.
Kwa Mkoa wa Mara program hii inatekelezwa chini ya uratibu wa kanisa la African Inland Church of Tanzania (AICT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Mara.
Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Madawati ya Jinsia ya Jeshi la Polisi, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya watu wenye ulemavu na viongozi wa dini.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa