Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Salum Hapi leo tarehe 5 Agosti, 2021 amezindua utoaji chanjo ya UVIKO 19 kwa wananchi wa Mkoa wa Mara katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa utoaji wa Chanjo Mheshimiwa Hapi amewataka wananchi kuondoa hofu, chanjo ni salama na wataalamu wa afya wamethibitisha hilo.
“Chanjo hizi ni salama na niwaombe wananchi tutumie fursa hii adhimu ambayo serikali ya awamu ya sita imeitoa kupata chanjo ili iweze kutukinga na UVIKO 19” alisema Mheshimiwa Hapi.
Aidha amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia diplomasia na kujenga hoja kufanikisha upatikanaji wa dozi milioni moja za awali ambazo serikali inazitoa bure kwa wananchi wake.
“Mheshimiwa Rais kwa mapenzi yake kwa watanzania ametutafutia chanjo hizi na sasa tunazipata bure na kuonyesha usalama wa chanjo hizi na yeye mwenyewe amechanjwa na anaendelea na jitihada za kutafuta chanjo nyingine” ameeleza Mheshimiwa Hapi.
Hata hivyo amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kuhusu chanjo hiyo kwa wananchi ili waweze kuchanja kwa hiari yao wenyewe.
“Ndugu zangu ugonjwa upo, na katika Mkoa wa Mara tunawagonjwa na wengine tumewapoteza, na hapa tunapakana nan chi za Kenya na Uganda zote zina wagonjwa, kwa hiyo ninawasihi tuchanjwe na kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga” amesema Mheshimiwa Hapi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela ameeleza kuwa kuwa kwa sasa Mkoa umepokea dozi 25,000 za chanjo na umetenga vituo 22 vya kutolea huduma ya chanjo kwa wananchi.
“Vituo hivi vinaweza kuongezwa kama kutaonekana kuna mahitaji ya kuongeza vituo zaidi ya hivi vya sasa ili wananchi wetu wapate chanjo kwa hiari na bila usumbufu” alisema Msovela.
Amewashukuru wananchi kwa mwitikio wao katika tukio la uzinduzi wa chanjo hiyo na kuwasihi watakaochanjwa kuendelea kuwashawishi wenzao wachanjwe.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Juma Mfanga ameeleza kuwa chanjo iliyopo kwa sasa ni aina ya Johnson inayotengenezwa na kampuni ya Johnson and Johnson na mtu anachomwa mara moja tu hairudii.
“Chanjo hii ya UVIKO 19 ni salama na imefanyiwa utafiti na wataalamu wa ndani na nje ya nchi na kuthibitishwa na mamlaka zetu kuwa ni salama kwa matumizi na zinatolewa kwa kutumia utaratibu wa kawaida wa chanjo” alisema Dkt. Mfanga
Dkt. Mfanga ameeleza kuwa katika suala la chanjo kuna hofu kuu mbili, moja ni hofu ya ubora na ufanisi wa chanjo na pili ni hofu hofu ya kuchoma sindano “niwatoe hofu kwa kuwa sindano hii ya chanjo haiumi sana na chanjo ni bora na inafanyakazi vizuri” alisema Dkt. Mfanga.
Aidha amewataka watu kutulia kidogo mara baada ya kuchomwa chanjo ya UVIKO 19 na kama mtu atapata maudhi yoyote baada ya chanjo ni hali ya kawaida kwachanjo yoyote arudi katika kituo alipopatiwa chanjo atapatiwa huduma.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na maambukizi ya UVIKO 19 hata baada ya kupatiwa chanjo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa