Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bwana Albert Gabriel Msovela amewataka wasimamizi wa huduma za Afya katika Mkoa wa Mara kutengeneza na kuja na mkakati madhubuti wa namna bora ya kuendelea kupambana na maambikizi ya uviko 19 katika Mkoa wa Mara.
Bwana Msovela ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Julai 2021 wakati wa kikao cha Timu ya Usimamizi wa Huduma za afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Waganga Musoma (COTC) ili kujadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na Uviko 19.
"Tunapotoka hapa kama wataalamu tunaohusika na masuala ya Afya ndani ya Mkoa inabidi tutengeneze mapendekezo na maazimio juu ya namna ya kupambana na Uviko 19 ili itusaidie katika kuona namna gani Mkoa unaweza kupunguza maambukiziā alisema Bwana Msovela na kuwataka waendelee kutoa huduma huku wakizingatia njia za kujikinga na maambukizi kwa sababu Watumishi wakichukua tahadhari hata wananchi wengine wataiga kutoka kwao maana mabadiliko yoyote yanaanza na watendaji kabla ya kufika kwa wananchi.
"Wataalamu tunapotoa huduma tuzingatie njia za kutumia katika kujiepusha na janga la Corona kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kukaa umbali unaohitajika na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kuhusu kujikinga na janga la Corona kwa kuendelea kufuata ushauri na elimu inayotolewa na wataalamu wa Afya ikiwemo kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala amewataka Watumishi wa sekta ya Afya kufanya kazi kwa upendo, ushirikiano na kuthaminiana kila mmoja katika nafasi yake ili katika utekelezaji wa majukumu kuwepo na mnyororo wa uelewa kuanzia ngazi ya juu hadi chini.
Aidha, amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha katika kila kituo Cha kutolea huduma za Afya kunafungwa mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato (GOTHOMIS) ili kuepusha mianya ya wizi na upotevu wa mapato ya serikali.
Awali akimkaribisha Katibu Tawala, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Frolian Tinuga amesema kuwa wagonjwa wa Corona katika Mkoa wa Mara wapo na jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kukabiliana na maambukizi zinafanyika hivyo kikao hiki kina lengo la kuweka mapendekezo na maazimio ya namna bora ya kuboresha zaidi mfumo na njia za kupambana na maambukizi kwa wananchi.
"Hakuna njia mpya za kujikinga na Uviko 19 zaidi ya zile zilizopo lakini kukutana kwetu inabidi tuweke maazimio na mikakati itakayoboresha na kutuwezesha kukabiliana na maambukizi kwa kuwafikia wananchi wote na kuwapatia elimu ya namna ya kupambana na ugonjwa huu.
Sambamba na hilo Dkt. Frolian amewaagiza wasimamizi wa huduma za Afya ngazi ya Halmashauri kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na Uviko 19 kwa kutembelea maeneo yenye mikusanyiko kutumia radio, magari ya matangazo pamoja na kuhakikisha katika vituo vyote vya kutokea huduma za Afya kunakuwepo njia zote za kujikinga na maambukizi ikiwemo uwepo wa maji ya kunawa na sabuni,vitakasa mikono pamoja na kusisitiza wahudumu wote na wananchi kuvaa barakoa pindi watoapo na kupata huduma.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
HatimilikiĀ©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa