Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhehsimiwa Ally Salum Hapi ameelezea mikakati ya Mkoa wa Mara yenye lengo la kuinua ufaulu wa wanafunzi katika mitahani ya kitaifa.
Mheshimiwa Hapi ameelezea mikakati hiyo leo tarehe 16 Julai 2021 wakati akipokea msaada wa vifaa vya elimu na afya uliotolewa na Benki ya NMB katika Shule ya Msingi Buhare iliyopo katika Manispaa ya Musoma.
“Mpango wa Mkoa ni kuhakikisha kuwa Mkoa wa Mara unashika nafasi ya tatu katika ufaulu wa mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha pili pamoja na kidato cha nne kwa mwaka 2021” alisema Mheshimiwa Hapi.
Ameeleza kuwa kutokana na ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka huu kwenye matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni, Mkoa wa Mara umeshika nafasi ya tatu kitaifa lakini mkoa umejiwekea lengo la kushika nafasi hiyo katika mitihani iliyobakia.
“Kuna kazi ya kufanya kwa sababu ufaulu wa wanafunzi wa shule ya msingi na kidato cha nne sio mzuri sana, walimu wasibweteke na Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara amepewa jukumu kusimamia mikakati yetu ya Mkoa ili iweze kutekelezwa ipasavyo” alisema Mheshimiwa Hapi.
“Msaada huu wa leo umekuja kutuongezea nguvu katika malengo yetu makubwa ya kukahikisha tunaifikia ndoto hii” alisema Mheshimiwa Hapi
Aidha amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuajiri walimu 6,000 na wengi wao wakiwa wa sayansi utaenda kupunguza tatizo kubwa la walimu hapa nchini.
Ameeleza kuwa Mkoa unachukua hatua mbalimbali kuhakikisha walimu wanafundisha wanafunzi madarasani na kuboresha usimamizi mzima wa elimu ili kuinua ufaulu wa wanafunzi.
Mheshimiwa Hapi amewataka wakurugenzi na maafisa utumishi wa Mkoa wa Mara kusikiliza kero za walimu katika maeneo yao ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu kwa wakati.
Aidha amewataka walimu kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuongeza juhudi katika ufundishaji, usimamizi wa utoro wa wanafunzi na kuwalea wanafunzi wawapo shuleni.
Mheshimiwa Hapi ameeleza kuwa Mkoa unampango wa kuweka vigezo vitakavyotumika kuwapima walimu wakuu na wakuu wa shule katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika Mkoa wa Mara.
“Mwalimu Mkuu tutamwekea vigezo vya kumpima ambavyo ni pamoja na ufaulu wa wanafunzi, usimamizi wa masuala ya taaluma, nidhamu na utunzaji wa mali na mazingira ya shule” alisema Mheshimiwa Hapi.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Musoma Mheshimiwa William Gumbo ameeleza kuwa Shule ya Msingi Buhare ambayo imepatiwa msaada na NMB ina changamoto kubwa ya mlundikano wa wanafunzi.
“Kwa sasa shule hii inawanafunzi zaidi ya 1,700 ambao wanafundishwa katika madarasa 22 yaliyopo katika shule hii na hamna eneo la ziada la kuongeza madarasa hapa” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Mheshimiwa Gumbo ameeleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo tayari Manispaa ya Musoma kwa kushirikiana na wadau wametafuta eneo la kujenga shule mpya ili kupanua miundombinu ya shule na msaada uliopatikana utatumika katika ujenzi wa shule hiyo.
“Tunashukuru kwa msaada huu wa mabati 300 ambayo yatatumika katika kuanza kujenga shule ya msingi mpya ambayo itapunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya Msingi Buhare” alisema Mheshimiwa Gumbo.
Mheshimiwa Gumbo ameeleza kuwa baada ya eneo la kujenga shule kupatikana, Diwani wa Kata ya Buhare na wadau wengine wamechangia mifuko 85 ya saruji na wiki ijayo wanampango wa kukutana na wadau wengine kwa ajili ya kuchangisha fedha za ujenzi wa shule hiyo.
Katika hafla hiyo ya kupokea msaada, Mkuu wa Mkoa aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Alfany Haule, Afisa Elimu wa Mkoa wa Mara Bwana Benjamin Oganga na Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, viongozi wa CCM, walimu na wanafunzi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa