Mkoa wa Mara umewataka wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini, unaotekelezwa na TASAF awamu ya tatu ambao hali zao kiuchumi zimeboreka kujiondoa kwenye mpango huo ili kutoa nafasi kwa kaya nyingine maskini zaidi ziweze kunufaika na mpango huo.
Hayo yameelezwa leo tarehe 19 Februari 2021 na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Mkoa utaendelea kufanya uhakiki wa kaya zote zinazonufaika na mpango huo na kaya itakayobainika kukosa sifa ya kuwa mlengwa wa mango wa TASAF itaondolewa katika mpango huu na wale watakaobainika kuwa awali hawakuwemo lakini kwa sasa wanakidhi vigezo wataingizwa” alisema Mheshmiwa Malima.
Mheshimiwa Malima ameeleza kuwa kwa Mwezi Februari 2021 halmashauri tisa za Mkoa wa Mara zimepokea jumla ya shilingi 1,794,074,000.00 kwa ajili ya malipo ya walengwa wa mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini wapatao 32,582.
Ameeleza kuwa Mkoa umeendelea kufanya uhakiki wa kaya zinazonufaika na hadi kufikia Februari 2021 kaya 6,998 ambazo awali ziliandikishwa zilipoteza sifa ya kuwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini kutokana na sababu mbalimbali.
Utekelezaji wa TASAF awamu ya tatu katika Mkoa wa Mara ulianza Julai 2014 kwa kuhusisha vijiji 354 na kaya 39,580 na hadi Februari 2021 serikali kupitia TASAF ilikwishakutoa shilingi bilioni 37,555,526,797.24 kwa ajili ya walengwa wa mpango huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa