Uongozi wa Mkoa wa Mara umewataka wanawake wote wenye changamoto mbalimbali za ukatili wa kijinsia kutoa taarifa kwa mamlaka na vyombo vya dola bila kujali makundi yanayowatishia kutoa taarifa ili kukomesha vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Vincent Naano katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani katika Manispaa ya Musoma yaliyofanyika katika Viwanja vya Mukendo, Musoma mjini tarehe 5 Machi 2020.
“Tunaelewa kuna watu wanawatishia msitoe taarifa, lakini nyie fikeni ofisi zote wa Wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na vyombo vya ulinzi na usalama ili kutoa taarifa na serikali ya Mkoa itashughulikia masuala yote ya unyanyasaji wa kijinsia ili kuhakikisha mnapata haki zenu” alisema Dkt. Naano.
Amesema kuwa pamoja na kuwa Mkoa umepiga hatua za kimaendeleo lakini kwa kiasi fulani bado Mkoa unachangamoto ya matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia na mpaka sasa kuna baadhi ya watu wanaowanyanyasa wanawake ikiwa ni pamoja na kuwazuia wanawake kufanyazi na kumiliki mali.
Wakati huo huo, mgeni rasmi wa sherehe hizo Mheshimiwa Gaudensia Kabaka, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Tanzania (CWT) amewahimiza wanawake wote kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ili kujiletea maendeleo wao wenyewe, familia zao na taifa kwa ujumla.
Aidha amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. “Wanawake wote wenye uwezo mchukue fomu za kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa mwaka 2020” alisema Mheshimiwa Kabaka.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa MKoa wa Mara, Bibi Karolina Mthapula amemshukuru sana mgeni rasmi kwa kukubali kuja katika hafla ya Siku ya Wanawake Duniani katika Manispaa ya Musoma.
Amewataka wanawake wote wachangamkie fursa mbalimbali zinazojitokeza kwa ajili ya kuongeza vipato vya familia zao na jamii kwa ujumla.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara
Anwani ya Posta: 13 Barabara ya Boma, P.o.Box 299 Musoma, 31101 Musoma, Mara
Simu: +255282622305
Simu:
Barua pepe: ras.mara@tamisemi.go.tz
Hatimiliki©2017 Mkoa wa Mara.Haki Zote Zimehifadhiwa